VIDEO: Simbachawene atoa maagizo matatu Uhamiaji, limo la uraia

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene

Muktasari:

Leo Jumamosi Februari 22,2020 Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene  ametembelea ofisi za Idara ya Uhamiaji zilizopo Kurasini jijini Dar es Salaam na kuwapa maagizo matatu anayotaka kuangaliwa na kuyafanyia kazi kwa weledi.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene  ametoa maagizo matatu kwa Idara ya Uhamiaji likiwamo suala la uraia.

Amesema baadhi ya watu wasio waaminifu  wamekuwa wakitumia mchakato huo kuwaumiza wengi wasipate haki zao za msingi.

Simbachawane alitoa maagizo hayo leo Jumamosi Februari 22, 2020 alipotembelea idara hiyo katika ofisi ndogo za makao makuu Kurasini Dar es Salaam, ikiwa ni ziara ya kwanza kutembelea taasisi hiyo iliyopo chini ya wizara yake.

Waziri huyo, aliyekuwa   Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) aliteuliwa Januari 23, 2020 kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais John Magufuli.

Katika maelezo yake, Waziri Simbachawane amesema uraia ni haki ya mtu mwenye sifa za kupata nafasi hiyo, lakini umekuwa ukitumia kinyume cha utaratibu na baadhi ya watu wasio na nia njema.

"Uraia umekuwa ukitumika kama silaha ya kuwaumiza wengine, nawasihi na kuwaomba mtafakari masuala haya. Jaribu kuwa makini huko mtaani watu wengine wakitaka kushindana na mtu kisiasa au kibiashara wanachomekea uraia," amesema Simbachawane.

Agizo la pili, kwa maofisa hao wa uhamiaji, Waziri Simbachawane amewataka kuangalia kwa umakini suala la vibali ya ukazi na ngazi mbalimbali akiwataka kuvitoa  bila kuwapo kwa urasimu huku akisema shughuli za jeshi hilo zimekuwa zikifanywa  mtaani na watu wasio watumishi.

"Jaribuni kufanya intelenjensia  ya kujua nani anayehusika kutumia jeshi la uhamiaji kama kichaka cha rushwa kwenye suala hili na Watanzania pia kuweni makini," amesema waziri huyo.

Simbachawane amewataka uhamiaji kulishughulikia suala la walowezi akisema inasikitisha pale mtu aliyeishi nchini kuanzia vizazi vitano hadi sita lakini akitaka kupata uraia kumbana na changamoto.

"Lakini mgeni aliyetoka nchi mbalimbali  anaweza kuupata uraia  kwa njia nyepesi. Ingawa suala la uraia lipo kisheria kunahitajika ushirikiano wakati wa kuchakata taarifa za kufanya uamuzi," alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala, Kamishna wa Uraia na Pasipoti , Gerald Kihinga alisema wameyapokea maagizo ya Simbachawane na kuahidi kuyafanyia kazi kwa uadilifu.

"Ametueleza masuala anayotaka kufanyia kazi  haraka kwa muda mrefu na mfupi. Kwa niaba ya wenzagu tutayatekeleza kwa ushirikiano bila kumuangusha," alisema Kihinga.