Watano waibuka washindi kampeni ya chanja kijanja

Maofisa waandamizi wa Benki ya Exim Tanzania wakiongozwa na Meneja Mwandamizi Huduma kwa wateja, Frank Matoro (Kushoto) wakionyesha mbele ya waandishi kadi za Mastercard zinazotumiwa na wateja wa benki hiyo wakati wa hafla ya kuwatangaza washindi. Wengine ni pamoja na Meneja Masoko wa Benki hiyo,  Mariam Mwapinga (Kulia)  na Ofisa Bidhaa za Rejareja, Callist Butinga.

Muktasari:

Washindi wa kampeni ya Chanja Kijanja wapatikana, wateja wa Exim wahamasishwa kuendelea kushiriki

Dar es Salaam. Benki ya Exim Tanzania imetangaza washindi watano wa mwezi katika kampeni yake ya 'Chanja Kijanja na Exim Mastercard' inayolenga kuhamasisha wateja wa benki hiyo  kutumia kadi zao za Mastercard katika manunuzi ya mtandaoni au kufanya malipo kupitia mashine za malipo (POS) katika maduka mbalimbali na maeneo mengine nchini.

Meneja Mwandamizi Huduma kwa wateja wa benki hiyo,  Frank Matoro amesema kampeni hiyo  inayoendelea ikishirikiana na Mastercard imeanza katikati ya mwezi Februari, 2020 ipo wazi kwa wateja wote wanaomiliki kadi za Exim Bank MasterCard, pamoja na wateja wote ambao wameomba au wataomba kadi mpya katika kipindi cha kampeni.

Amewataja washinidi hao ni Fahim Mohamed, Baraka Rom Kimaro (Dar es Salaam),   Hendrick  Hopley (Arusha),   Humphrey Henry ( Mbeya) na Amani Makungu (Zanzibar) ambao kila mmoja atazawadia simu janja (smartphone).

Amesema "Ifahamike kwamba mpaka sasa wateja 40 wameshajishindia vocha za manunuzi zenye thamani ya sh 50,000 kila mmoja na zinaendelea kutolewa kila wiki. Pia tunatoa zawadi kama hizi za leo za simu janja kwa washindi watano kila mwezi hadi mwisho wa mwezi Aprili, 2020 kwani ndio tutakuwa tunafika kilele cha kampeni yetu’’

“Katika kuhitimisha kampeni hii tutatoa zawadi kubwa zaidi kwa washindi watatu ambapo mshindi wa kwanza ataenda Dubai, mshindi wa pili ataenda Cape Town, Afrika Kusini na wa tatu ataenda visiwa vya Zanzibar. Washindi hao pamoja na wenza wao watagharamiwa gharama zote ikiwemo Visa, Tiketi ya Ndege pamoja na pesa za matumizi.'' amefafanua