Wabunge wa Tanzania waliosafiri nje ya nchi kupimwa kabla ya kuingia bungeni

Muktasari:

Vikao vya mkutano wa 19 wa Bunge vinatarajiwa kuanza tarehe 31/03/2020

Dodoma. Bunge la Tanzania limetangaza kuwa wabunge wote waliofanya safari za nje ya nchi kwa siku za karibuni watahitajika kupitia katika zahanati za Bunge kupimwa ili kujiridhisha kama hawana virusi vya ugonjwa wa corona kabla ya kuingia bugeni kuendelea na shughuli zao.
Taarifa hiyo ya Bunge imetolewa leo Jumatatu, Machi 16, 2020 ikiwa tayari Tanzania imethibitisha kuwapo kwa mgonjwa mmoja wa virusi hivyo.
Katika taarifa hiyo imeeleza kuwa katika vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza Machi 31, 2020 kutakuwa na miongozo mbalimbali itakayotumika kama njia ya kujikinga na ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi duniani.
Baadhi ya miongozo hiyo ni pamoja na kupunguza idadi ya wageni ambao wamekuwa wakialikwa bungeni kwa makundi, kusitishwa kwa safari za nje za kikazi kwa wabunge wa Tanzania hasa kwenda nchi ambazo ugonjwa huo unasambaa, vikao vyote vya kamati za kufanyika katika kumbi za Bunge huku wakilazimika kupunguza idadi ya wajumbe ili kuepuka msongamano.
Vilevile taarifa hiyo imeeleza kuwa kutakuwa na vifaa maalumu vya kuoshea mikono nje ya ukumbi wa Bunge kwa ajili ya wabunge na wageni wote.  
Bunge la Tanzania limesema litaendelea na vikao vyake kama vilivyopangwa mpaka pale itakapotoka taarifa nyingine kuhusu suala hilo.