Kongamano la kilimo lapigwa stop kuepuka maambukizi ya corona

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga

Muktasari:

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga  amesitisha kongamano la vijana kuhusu kilimo lililokuwa lifanyike leo  Jumanne Machi 17, 2020 Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kwa sababu ya kudhibiti kuenea kwa  maambukizi ya virusi vya corona.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga  amesitisha kongamano la vijana kuhusu kilimo lililokuwa lifanyike leo  Jumanne Machi 17, 2020 Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kwa sababu ya kudhibiti kuenea kwa  maambukizi ya virusi vya corona.

Uamuzi huo unatokana na maelekezo yaliyotolewa na Serikali  kuchukua tahadhari ya mikusanyiko ya watu wengi kuepusha hatari ya kusambaa kwa maambukizi hayo.

Jana Wizara ya Afya iliripoti kuwepo kwa mgonjwa mmoja wa kwanza kwa corona nchini Tanzania.

Ugonjwa huo ulioanzia katika mji wa Wuhan, China Desemba, 2019 na baadaye kuanza kusambaa nchi mbalimbali umesababisha vifo vya watu zaidi ya 4,500 huku Tanzania ikiwa nchi ya tatu Afrika Mashariki kuwa na mgonjwa wa corona baada ya Kenya na Rwanda. Baadhi ya nchi za Afrika zenye wagonjwa wa corona ni Afrika Kusini, Misri na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Taarifa iliyotolewa jana jioni na Wizara hiyo imewataarifu   wadau wote wa sekta ya kilimo na vijana waliopanga kushiriki kongamano hilo kujadili fursa za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kanda ya Dar es Salaam inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara kutohudhuria  kongamano hilo hadi watakapopewa taarifa  baadaye.

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa rai kwa Watanzania kuchukua tahadhali  na vihatarishi vinavyoweza kusababisha maambukizi ya corona kwa kuepuka mikusanyiko ya watu wengi isiyo ya lazima.

Hasunga amewataka wakulima na vijana wote nchini kuendelea kuchukua hatua za tahadhali kwa kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya   ili kuthibiti maambukizi ya virusi hivi vya corona nchini.