Tofauti kati ya Covid 19, milipuko mingine ya corona

Mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona duniani unaosababisha ugonjwa wa covid-19, sasa ndio tishio linalosababisha nchi mbalimbali kutoa mazuio katika maeneo yanayokutanisha watu wengi.

Mpaka jana maambukizi ya virusi hivyo yamewakumba watu 294,110, huku waliofariki dunia wakiwa 12,944.

Nchi 186 duniani zimeshapata maambukizi ya virusi hivyo vilivyoanzia katika mji wa Wuhan nchini China Desemba mwaka jana.

Kutokana na hali ilivyo ni muhimu kufahamu kwa undani juu ya virusi hivyo ambavyo mpaka sasa vinaendelea kuitikisa dunia.

Mlipuko wa ugonjwa unaotokana na virusi vya corona si mara ya kwanza kutokea duniani, kwani miaka ya nyuma kumekuwapo na magonjwa yanayotokana na virusi hivyo kama Mers na Sars yaliyoibuka mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Corona ni jamii kubwa ya virusi vinavyosababisha maradhi kwa wanyama na binadamu.

Kwa binadamu, jamii kadhaa za virusi vya corona vinafahamika kusababisha maambukizi kwenye njia ya hewa na mfumo wa upumuaji. Maradhi yaliyowahi kusababishwa na virusi vya corona ni Mers na Sars.

Tofauti ya ugonjwa wa Covid 19 na magonjwa mengine ni kuwa ugonjwa huu unasambaa kwa haraka zaidi.

Tangu Desemba mwaka jana hadi Machi 19 mwaka huu, ugonjwa wa Covid 19 ulikuwa umeshaathiri watu zaidi ya 200,000, lakini mlipuko wa ugonjwa wa Sars ulichukua miezi sita kuathiri watu zaidi 5,000.

Mlipuko wa ugonjwa wa Sars uliotokea China kuanzia Novemba 2002 na kuisha Julai 2003, ulisababisha vifo vya watu 774 na ulisambaa katika nchi 29. Watu 8,098 walipata maambukizi.

Kwa ugonjwa wa Mers uligundulika kwa mara ya kwanza nchini Saudi Arabia, Aprili 2012 mpaka Septemba 2019 na kuathiri zaidi ya watu 2,400 katika nchi 27, huku vifo vikiwa 912.

Akielezea tofauti za ugonjwa wa Covid 19 na magonjwa mengine, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Mahamed Janabi, aliwataka wananchi kutolinganisha mafua mengine kama flu na ya Covid 19.

Alisema tafiti zote zilizofanyika hivi karibuni zinaonyesha kuwa ugonjwa wa Covid 19 ni hatari zaidi ya mara 10 ya flu ya kawaida hasa ukizingatia tangu ugundulike hakuna dawa wala chanjo, lakini magonjwa mengine kama mafua yana chanjo.

“Mimi, wewe tunaugua mafua mara kadhaa kwa mwaka na yanakuja kwa msimu. Yanaweza yakaanza Desemba mpaka mwezi wa tatu au wa nne yakapotea, hivyo miili yetu imeshajenga kinga ya flu ya kawaida. Huu ugonjwa ndio kwanza umeanza, miili yetu imestukizwa na hivi virusi.

“Ukitazama flu ya kawaida inashambulia watoto na watu wazima, lakini vifo tunavyoviona kwa wenzetu, inashambulia watu wazima zaidi wenye umri wa miaka 70, 80 na sababu zaidi ni nguvu zao zinakuwa ndogo,” alisema.

Alisema sababu nyingine ambayo nayo ni hatari ni kwamba mtu akiwa na magonjwa mengine kama tatizo la moyo, shinikizo la damu, saratani, kisukari, uuaji wake upo karibu asilimia 10.

Dk Janabi alisema kama mtu ana ugonjwa huo na akikohoa bila tahadhari, virusi hukaa hewani kwa muda mchache, lakini vikitua kwenye meza, chombo cha plastiki na milango vina uwezo wa kukaa mpaka siku tatu, hivyo mtu mwingine akigusa anapata maambukizi.

Pia alisema kuna watu wengine wanapata maambukizi, lakini hawaonyeshi dalili zozote na kwamba wana uwezo wa kuambukiza mtu mwingine kuanzia siku ya saba mpaka ya 14.

“Kila mtu aliyeambukizwa huu ugonjwa ambaye hana dalili yoyote anaweza kumbukiza watu wengine kati ya wanne hadi sita,” alisema.

Naye Dk Elly Josephat kutoka Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), akihojiwa katika kituo kimoja cha televisheni nchini alisema mlipuko wa virusi vya corona si wa kwanza kutokea na kwamba virusi vimekuwa na tabia ya kubadilika.

“Corona zipo za aina nyingi ambazo zimeshatokea zamani lakini tofauti na hii, zile hazikusambaa sana. Mfano mwaka 2003 kirusi cha corona aina ya Sars nayo ilitokea China na uzuri waliwahi kudhibiti. Ilianza Machi mpaka kufikia Juni waliweza kudhibiti.

“Tofauti na milipuko iliyotangulia, huu unasambaa kwa haraka zaidi, hivyo ni muhimu kufahamu jinsi ya kujikinga,” alisema Dk Josephat.

Uganda wafanya utafiti

Maabara ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Makerere, chuo cha tiba ya mifugo, imegundua aina tofauti za virusi vya corona katika sampuli zilizokusanywa kutoka kwa popo nchini humo.

Profesa Denis Byarugaba, mwanasayansi aliyeongoza utafiti katika maabara, wakati akihutubia kuhusu virusi vya corona huko Kampala hivi karibuni alisema walifanya uchunguzi kadhaa miaka iliyopita na kubaini virusi vilivyozoea kuishi kwa binadamu.

“Tumechunguza sampuli 16,000 na kuona ongezeko la kiwango cha virusi vya corona kwa asilimia 0.6,” alisema.

Profesa Byarugaba alisema wakati wa milipuko ya virusi hivyo walifanya utafiti kwa popo 500 na kubaini kuwapo kwa virusi vya aina nyingi vya corona.

“Kwa kushirikiana na wataalam mbalimbali tulifanikiwa kuwatenga virusi hivyo kutoka kwa popo,” alisema.

Mtaalam huyo pia alisema jaribio lingine lilifanyika kwa ngamia kutoka Karamoja.

“Tulitafanya utafiti kwa ngamia. Tulipima ngamia 500 na kubaini asilimia 70 walikuwa na virusi hivyo,” alisema.

Mtafiti huyo alisema kwamba kuna haja ya kuongeza juhudi za kutafuta virusi hivi katika wanyama wengine kwa malengo bora ya uchunguzi.

Mtaalam mwingine katika chuo hicho, Dk Sylvia Baluka ambaye pia ni rais wa Chama cha Mifugo cha Uganda (UVA), alisema kwamba magonjwa mengi yanayoathiri binadamu hutoka kwa wanyama, ni wanyama wa mifugo.

Alisema Serikali inapaswa kutoa fedha zaidi za kuimarisha utafiti, ufuatiliaji na kanuni za bidhaa za mifugo kwa lengo la kuzuia magonjwa haya kabla ya kusambaa kwa watu.

Profesa Pontiano Kaleebu ambaye ni mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Virusi Uganda (UVRI), alisema virusi vya corona vimekuwapo nchini Uganda kwa muda mrefu.

“Watu kadhaa wameathirika na virusi hivi. Ikiwa umewahi kupata homa na kikohozi kifupi, inaweza kuwa ni kwa sababu ya virusi hivyo,” alisema Kaleebu.

Pia alisema virusi hivyo vipo hata kwa kuku, ndege na wanyama wengine.

“Virusi viligunduliwa kwa mara ya kwanza miaka ya 1960, viliathiri ndege na wanyama,” alisema na kuongeza kuwa virusi hivyo vimekuwa hatari kwa sababu vimetoka kwa mnyama na kwenda kwa binadamu.

“Aina hii ya virusi inaongoza kwa kuambukizwa, inaweza kuathiri mapafu. Ni virusi hatari zaidi kuliko vingine,” aliongeza.

Kwa nini watu hupona bila dawa?, Profesa Kaleebu alisema mwili una nguvu ya asili kushinda mapambano dhidi ya virusi.

“Kama vile watu hupata homa na kupona, ni sawa na coronavirus. Watu wengi (asilimia 80 ya walioambukizwa) hupona, watu wanaokufa ni wazee,” alisema.