Uwezeshaji wanawake kisheria ni silaha muhimu katika kukabiliana na umaskini

Muktasari:

Huu ni mpango kabambe unaosaidia maelfu ya Watanzania wasioweza kumudu gharama za huduma za msaada kisheria kupata haki zao tofauti na awali ambapo upatikanaji wa haki hasa kwa wanawake

Dar es Salaam. Uwezeshaji wanawake kisheria ni hatua muhimu katika kuwawezesha kujua haki zao katika kupambana na umaskini wa kipato.
Hayo yamesemwa na msaidizi wa Kisheria wa shirika la Kaengea Environment Society (KAESO), Filbert Milambo, alipokuwa anaeleza jinsi ambavyo shirika lao limesaidia katika kupata haki ya kisheria kwa Lilian Ally kutoka wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa.
“Kisa cha Lillian kuzulumiwa haki yake kinaakisi mazingira ya wanawake wengi ambao siku hadi siku wanagundua kuwa kuna maisha mazuri pale ambapo wanajua haki zao, wanaweza kuzipata na wanabadili maisha yao kwa kuzitumia,” alisema Milambo.
Lilian anapiga hatua kimaisha pamoja na watoto wake baada ya kutumia vyema uwepo wa wasaidizi wa kisheria na hii ni nafasi kwake kujikwamua kutoka kwenye maisha magumu yanayochangiwa na umasikini.
Wasaidizi wa kisheria wapatikana nchini nzima katika kila mkoa na wilaya chini ya progamu inayofadhiliwa na Legal Services Facility (LSF). Maelfu ya wakazi hususani wa pembezoni wamepatiwa msaada na elimu ya kisheria bila malipo.
“Huu ni mpango kabambe unaosaidia maelfu ya Watanzania wasioweza kumudu gharama za huduma za msaada kisheria kupata haki zao tofauti na awali ambapo upatikanaji wa haki hasa kwa wanawake ulikuwa jambo gumu sana,” alisema Filbert
Lillian ameweza kufanya biashara hizi na kumudu kuendesha maisha yake na kulea watoto wake wawili baada ya kufanikiwa kupata talaka na baadhi ya mali za familia ambazo awali mume wake aliamua kuziuza bila kumshirikisha na hivyo kukosa haki yake.
Wasaidizi hawa wa kisheria wana utaratibu wa kuitisha mikutano ya hadhara na kutoa elimu kuhusu majukumu yao na kutoa msaada wa kisheria bure, na hivi ndivyo Lilian alivyofahamu kazi zao na hivyo kutafuta msaada kwao.
Huku akijitahidi kukabiliana na hali hii ngumu baada ya kuachwa na mume wake na njia nyingine za kutafuta haki yake kushindwa kuzaa matunda Lillian alitafuta suluhisho kwa kuamua kufikisha suala lake mikononi mwa wasaidizi wa kisheria kwa kusaidiwa na Wilbroad Nzumi, mwenyekiti wa kijiji chake.
Nzumi amesaidiana na wasaidizi hawa wa kisheria kwenye matukio mengi na ujio wa Lillian haukuwa jambo geni kwao.
“Mambo ambayo mume wa Lilian alituhumiwa nayo yalionekana kuwa mazito na kwa kawaida yetu tulikutana nao kwa pamoja huku mwenyekiti wa kijiji akiwepo na kuzisikiliza pande zote mbili. Ingawa hayakuwa mazungumzo rahisi lakini tulitumia nafasi ile kuwaelimisha juu ya sheria na haki ndani ya wigo wa ndoa.
Kwa sababu ndoa yao ilifungwa Kiislamu Hassan alipata nafasi ya kueleza msimamo wake na suluhisho likawa kukubali kutoa talaka ili Lillian aweze kuendelea na maisha bila usumbufu. Hassan alikubali na siku chache baadaye alirudi na kukabidhi talaka hiyo,” alisema Milambo.
Hatua zaidi za kisheria zilifuata na kumuwezesha Lillian kurudishiwa vitu vingine ambavyo Hassan alivichukua zikiwemo samani na vifaa vya uvuvi na hivi ndivyo vilivyomuwezesha Lillian kuwa na msingi wa kuanza kuendehsa maisha yake mwenyewe na kuwalea watoto wake.
 Alidai na kulipwa pia fedha ambazo Hassan alijipatia kutokana na kuuza nyumba waliyokuwa wakiijenga ambayo haikuweza kukamilika.