Mbowe amtimua Mbatia, wabunge wa CUF katika baraza mawaziri kivuli

Dodoma/Dar. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imefanya mabadiliko ya Baraza Kivuli la Mawaziri na kuwaondoa wabunge wa CUF na NCCR-Mageuzi na kubaki wa Chadema pekee.

Mabadiliko hayo yanakuja ikiwa ni mkutano wa mwisho kabla ya Bunge kuvunjwa na kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mabadiliko hayo, Kiongozi wa Kambi hiyo, Freeman Mbowe alisema mazingira ya kisiasa yamemlazimisha kufanya mabadiliko hayo ili kuwa na kambi rasmi yenye kufanya kazi kwa umoja.

Kuhusu kuwaacha wabunge wa CUF, Mbowe alisema wakati akiunda baraza hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2015, Chadema na CUF walikuwa wanashirikiana lakini baada ya mgogoro uliotokea na kuigawa CUF makundi mawili ya Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba yamechangia kuwaweka kando.

Mbowe alisema baada ya mgogoro huo kumalizika, kuna wabunge wako ‘CUF Lipumba’ na wengine CUF/ACT- Wazalendo ambako Maalim Seif alihamia na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, jambo ambalo linawawia vigumu kufanya nao kazi.

“Chadema tulikuwa tunafanya kazi na CUF ile ya Maalim Seif, lakini baada ya kile kilichotokea, CUF imebaki moja ya Lipumba ambayo sisi hatufanyi nayo kazi na kwa mazingira kama hayo ndiyo yamesababisha kuwaacha katika baraza kwani siwezi kuingilia mambo ya chama kingine,” alisema mwenyekiti huyo wa Chadema.

Akigusia suala la kumwacha mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ambaye pia ni mbunge wa Vunjo, James Mbatia kwenye baraza hilo, Mbowe alisema, “Mbatia nilimuuliza kuwa nataka kufanya mabadiliko ya baraza utakuwa tayari kuendelea kufanya kazi, akasema atafurahi kama nitamwacha, kwa hiyo ndicho kilichotokea.”

Jitihada za kumpata Mbatia azungumzie mabadiliko hayo hazikuzaa matunda kwani katika viwanja vya Bunge hakuweza kupatikana na simu zake za kiganjani nazo zilikuwa zikiita bila kupokewa.

Katika mabadiliko Mbowe ameunda baraza hilo kama ifuatavyo: Esther Bulaya (Mnadhimu wa Upinzani Bungeni), Jaffary Michael (Ofisi ya Rais Tamisemi), Ruth Mollel (Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora), Tunza Malapo (Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira), Esther Bulaya (Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Ajira na Vijana), Pascal Haonga (Waziri wa Kilimo) na Dk Immaculate Semesi (Mifugo na Uvuvi).

Wengine ni Qambalo Qulwi (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Halima Mdee (Fedha na Mipango), Grace Tendega (Nishati), John Heche (Madini), Salome Makamba (Katiba na Sheria), Peter Msigwa (Maliasili na Utalii), Gibson Meiseyeki (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Godbless Lema (Mambo Ndani).

Mawaziri wengine ni Esther Matiko (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Wilfred Lwakatare (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), David Silinde ( Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Susan Lyimo (Elimu, Sayansi na Teknolojia).

Wengine ni Cecilia Paresso (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), Zubeda Sakuru (Maji na Umwagiliaji) na Joseph Mbilinyi (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo).

Naibu mawaziri ni Sophia Mwakagenda (Ofisi ya Rais Tamisemi), Zainabu Mussa Bakari (Ofisi ya makamu wa Rais-Mazingira na Muungano), Frank Mwakajoka (Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Ajira na Vijana), Anatropia Theonest (Kilimo), Lucy Megeleli (Mifugo na Uvuvi) na Susan Kiwanga (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano). Naibu mawaziri wengine ni Catherine Ruge (Fedha na Mipango), Jesca Kishoa (Nishati), Joseph Haule (Madini), Sabrina Sungura (Katiba na Sheria), Joyce Mukya (Maliasili na Utalii), Peter Lijualikali (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Rhoda Kunchela (Mambo ya Ndani) na Upendo Peneza (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa).

Wengine ni Grace Kiwelu (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Lucy Owenya (Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Yosepher Komba (Elimu, Sayansi na Teknolojia) na Hawa Mwaifunga (Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto), Lucy Mlowe (Maji na Umwagiliaji) na Devotha Minja (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.