VIDEO: Dk Bashiru ateta na mabalozi kuhusu uchaguzi

VIDEO: Dk Bashiru ateta na mabalozi kuhusu uchaguzi

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Bashiru Ally alisema Balozi Wright aliomba kukutana na mgombea urais kutoka CCM, John Magufuli na wa urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, lakini haikuwezekana kutokana na ugumu wa ratiba zao.

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali jana alikutana na mabalozi kadhaa wanaoziwakilisha nchi zao, akiwamo wa Marekani, Donald Wright na kujadiliana mambo kadhaa ya kudumisha uhusiano na kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28.

Wright, ambaye ubalozi wake umepewa kibali cha uangalizi wa uchaguzi, alifika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es Salam jana saa 3:30 asubuhi na kufanya mazungumzo kwa saa mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Bashiru Ally alisema Balozi Wright aliomba kukutana na mgombea urais kutoka CCM, John Magufuli na wa urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, lakini haikuwezekana kutokana na ugumu wa ratiba zao.

“Amenieleza kuwa ofisi yake imepewa kibali cha kuangalia uchaguzi. Alitaka kuzungumza na wagombea wetu wa Zanzibar na Muungano. Nikamweleza kuwa nimetumwa mimi kuzungumza nao kwa niaba yao kwa sababu wapo katika kampeni,” alisema Dk Bashiru.

Balozi huyo aliandika katika akaunti yake ya Twitter baadaye kuwa amekutana na Dk Bashiru ikiwa ni sehemu ta mpango wake wa kukutana na vyama vya siasa.

Tukio hilo limekuja wakati ubalozi huo ukiwa umetoa taarifa kuwa inafuatilia kwa makini uchaguzi wa Tanzania na Marekani haitasita kuchukua hatua dhidi ya watu ambao watahusika katika kuuvuruga.

“Hatutasita kufikiria kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaobainika kuhusika katika vurugu na machafuko yanayohusu uchaguzi au kukwaza mchakato wa kidemokrasia,” ilisema taarifa hiyo.

Uchaguzi kuwa huru

Akizungumzia mazungumzo yao, Dk Bashiru alisema amemhakikishia balozi huyo kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

“Nimemhakikishia kwamba nchi yetu itaendelea kuwa na amani, siku ya kupiga kura na baada ya matokeo na yeye akasema nchi yake ingependa kuona tunaendesha uchaguzi katika hali ya amani, usalama, haki na uhuru,” alisema.

Wajadili mambo manne

Mbali na masuala ya uchaguzi, Dk Bashiru alisema walijadiliana na Balozi Wright mambo manne, likiwamo la afya, hasa katika kukabiliana na maradhi ya Ukimwi, malaria na mchango wa Marekani katika maeneo hayo.

“Kitu cha pili ni uwekezaji na ametaka kuboresha uhusiano wetu katika uwekezaji na biashara na maeneo mbalimbali, akiamini kwamba Tanzania ina maeneo mengi ya ushirikiano.

“Tatu amezungumzia kuhusu hifadhi ya mazingira, maeneo ya wanyamapori pamoja na uhusiano katika sekta ya utalii, pamoja na kuwepo na changamoto za corona,’’ alisema Dk Bashiru.

Eneo la nne ni uhusiano kati ya watu wa Tanzania na Wamarekani. Pia uhusiano katika ya masuala ya demokrasia, uhamiaji, udugu na utamaduni.

Mbali na CCM, Balozi Wright pia ameshakutana na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu na mgombea urais wa Zanzibar (ACT-Wazalendo), Maalim Seif Sharif Hamad.

Mabalozi wengine

Dk Bashiru pia alikutana balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu ambapo pamoja na mambo mengine walijadili ushirikiano wa kiuchumi na masuala ya siasa kati ya CCM na vyama vya ODM na Jubilee vya Kenya.

“Katika Afrika Mashariki nchi zilizoingia katika uchumi wa kati ni Kenya na Tanzania, kwa hiyo inamaanisha kimataifa sisi tuna majukumu ya kushirikiana,’ ’alisema.

Pia alikutana na Balozi Monica Patricio wa Msumbiji ambaye alisema nchi yake inafuatilia Uchaguzi Mkuu akitarajia utakuwa wa amani.

Ugumu ratiba ya Magufuli

Kuhusu Magufuli, Dk Bashiru alisema ametingwa pia na shughuli za urais.

“Rais Magufuli amekuwa na kazi nyingi za uongozi wa nchi na kampeni. Nikamweleza ndiyo maana hakuweza kwenda baadhi ya mikoa kama ya Pemba, Ruvuma, Katavi, Rukwa, Lindi, Mtwara na Morogoro.

Alisema ndani ya siku 60 za kampeni, wagombea hao wanatakiwa kutembelea mikoa 32 ya kichama, jambo alilosema limemuwia vigumu kutokana na shughuli nyingi.

“Mtindo wake wa kwenda kwa gari ili aweze kujionea na kuzungumza na wananchi katika maeneo ya vijijini, umetunyima muda na nafasi,” alisema.

Alisema wamegawana maeneo ya kampeni na mgombea mwenza, Samia Suluhu na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa kufikia mikoa yote.

“Kwa sasa ratiba ya mwenyekiti, akishatoka Dar es Salaam, atakwenda Pwani, atakwenda Tanga, Arusha, Manyara kisha ataingia Dodoma.