Sinema ya Maalim Seif na Jecha Zanzibar inavyochukua nafasi Guinea

Muktasari:

Cellou Dalein Diallo, mgombea urais wa Guinea kwa tiketi ya chama cha UFDG, ameshajitangaza mshindi katika uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita.

Cellou Dalein Diallo, mgombea urais wa Guinea kwa tiketi ya chama cha UFDG, ameshajitangaza mshindi katika uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita. Juzi (Jumatatu), siku moja baada ya uchaguzi kufanyika, Diallo ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo mwaka 2004-2006, alisema yeye ndiye mshindi.

Haitoshi, Diallo aliwataka wananchi wapenda demokrasia na watetezi wa Katiba nchini Guinea, kuungana ili kuulinda ushindi ambao ameupata.

Diallo alisema: “Pamoja na mambo mengi kutokuwa sawa kwenye uchaguzi huu, nimeweza kushinda kwenye duru ya kwanza.

Nawaomba wananchi wenzangu wa Guinea, wapenda amani na haki, tuulinde ushindi huu wa kidemokrasia.”

Baada ya tangazo hilo la Diallo kwa wanahabari, wafuasi wake walimiminika barabarani na kushangilia. Maneno “Diallo Rais”, yakiwa ndio wimbo mkuu. ___Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wakisherehekea kile ambao walikiamini ni ushindi wa Diallo.

Alasiri ya Jumatatu, ikiwa ni takriban dakika 120 tangu Diallo alipojitangaza mshindi, Makamu wa Rais wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) nchini Guinea, Bakary Mansare, alisema kuwa kinachoitwa ni ushindi wa Diallo kimeharakishwa mno na hakikubaliki.

“Sio jukumu la mgombea au mtu yeyote kujitangaza mshindi nje ya chombo kilichoundwa kisheria,” alisema Mansare.

Tangazo la Diallo kuwa yeye ndiye mshindi na kanusho la Mansare, linaweza kukumbusha sinema ya Uchaguzi Mkuu Tanzania mwaka 2015 upande wa Zanzibar. Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Seif Sharif Hamad, alijitangaza mshindi kwa zaidi ya asilimia 50, dhidi ya Rais aliyekuwa anawania muhula wa pili, Dk Ali Mohamed Shein.

Tangazo la Seif kuwa ndiye mshindi, lilimuibua aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, aliyeamua kufuta matokeo yaliyokuwa yakiendelea kutangazwa, kisha ukatangazwa uchagauzi wa marudio uliofanyika Machi 20, 2016, ambao Seif aliususia.

Diallo, hakusema alishinda kwa idadi ipi ya kura, badala yake alisema kuwa kwa majumuisho ambayo chama chake kiliyafanya, tayari ameshashinda.

Lipo swali, je, CENI wakithibitisha ushindi wake watamtangaza? Na kama asipotangazwa nini kitatokea? Au CENI watafuta matokeo ili kukamilisha sinema kama ya Zanzibar mwaka 2015?

Hali ya mchuano

Katika uchaguzi wa sasa Guinea, Diallo, anachuana kwa ukaribu na Rais aliye madarakani, Alpha Conde. Si mara ya kwanza Conde na Diallo kupepetana kwenye uchaguzi. Mwaka 2010 na 2015, walikutana. Mara zote hizo mbili Conde aliibuka mshindi. Malalamiko ya Diallo ni kuwa awamu zote hizo aliibiwa kura.

Mwaka 2010, Diallo aliongoza kwa kura katika awamu ya kwanza. Alipata asilimia 40, wakati Conde alijikusanyia asilimia 18. Kwa vile hakaukuwa na mgombea aliyepata kura zaidi ya asilimia 50, ilibidi uchaguzi urudiwe kwa wagombea wawili; Diallo na Conde. Mwisho, Conde alishinda kwa kupata asilimia 52.5, Diallo asilimia 47.5.

Mwaka 2015, Conde kupitia chama cha RPG, alishinda urais kwa kupata kura asilimia 58, wakati Diallo alipata asilimia 31. Hata mwaka huu, kulingana na matakwa ya Katiba ya Guinea, endapo hakutakuwa na mgombea atakayevuka asilimia 50 ya kura, uchaguzi utarudiwa kwa mshindi wa kwanza na wa pili ili mshindi awe na uhalali wa wapigakura zaidi ya asilimia 50.

Uchaguzi mwaka huu sio Conde na Diallo pekee wanaowania urais, bali kuna wagombea wengine 10 wameiomba nafasi hiyo; Ousmane Kaba wa chama cha Democrats for Hope, Kabelele Abdoul Camara (Guinean Rally for Development), Abdoulaye Abe Sylla (New Generation for the Republic), Makale Traore (Party of Civic Action for Work) na Makale Camara wa Front for National Alliance.

Wengine ni Moro Mandjouf Sidibe (Alliance for the Forces of Change), Bouya Konate (Union for the Defence of Republican Interests), Laye Souleymane Diallo (Party of Freedom and Progress), Ousmane Dore (National Movement for Development) na Abdoulaye Kourouma wa Rally for Renaissance and Development.

Hali ni tete

Utete wa hali ya kisiasa Guinea unaanzia Agosti, mwaka jana, Chama tawala kwa kushirikiana na asasi za kiraia, walianzisha muungano wa kupigania katiba mpya. Ukaitwa Umoja wa Kidemokrasia kwa ajili ya Katiba Mpya (CODENOC).

Vyama vya upinzani na asasi nyingine za kiraia, wakaunda muungano wao. Wakauita Umoja wa Kitaifa wa Kuilinda Katiba (FNDC). Oktoba 7, mwaka jana, FNDC waliitisha maandamano ya kupinga mabadiliko ya Katiba, kwa kile walichoeleza kuwa shabaha kuu ilikuwa kumfanya Conde kujiongezea muhula wa kukaa madarakani.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, lilitoa ripoti hivi karibuni kuwa kati ya Oktoba mwaka jana na Julai mwaka huu, watu zaidi ya 50 walipoteza maisha Guinea kufuatia maandamano yaliyoanza Oktoba 14, mwaka jana, kupinga mabadiliko ya katiba.

Kwa kifupi, tangu FNDC walipoitisha maandamano ya kupinga mabadiliko ya katiba, Guinea hapajatulia. Mapambano ya waandamanaji na dola yamekuwa hayakomi. Kwa mujibu wa FNDC, watu waliopoteza maisha kati ya Oktoba mwaka jana na Septemba mwaka huu ni zaidi ya 90.

Desemba mwaka jana, Rais Conde aliiweka hadharani rasimu ya Katiba mpya. Machi 22, mwaka huu, wananchi wa Guinea walipiga kura kwa wingi kupitisha Katiba mpya ambayo pamoja na mambo mengine, iliondoa kipengele cha ukomo wa wa mihula miwili ya uongozi. Ni kwa kuondolewa kwa kipengele hicho, ndipo Conde alipata fursa ya kugombea.

Kutokana na hali ya maandamano, ilidhaniwa hata uchaguzi wenyewe usingefanyika. Hata hivyo, upepo ulibadilika baada ya Diallo, kinara wa wa FNDC, kubadili msimamo na kutangaza kumkabili Conde kwenye sanduku la kura.

Ni hali hiyo inayofanya hali iwe tete Guinea. Siku ya uchaguzi (Jumapili iliyopita), mvua ilinyesha kubwa asubuhi. Ilipokatika, mamilioni ya Waguinea walijitokeza kwenda kupiga kura. Kwa jumla, hali ya wakati wa upigaji kura na hata kuhesabu imekuwa ya amani. Shaka ipo kipindi cha majumuisho ya mwisho ya CENI na utoaji wa matokeo.

Waziri wa Usalama wa Guinea, Albert Damantang Camara, aliliambia Shirika la Habari la AFP, Jumatatu iliyopita kuwa siku ya upigaji kura hakukuwa na tukio kubwa, ingawa kuna wahuni wachache walifanya jaribio la kushambulia vikosi vya usalama.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu jijini Conakry, Patrice Vahard, alisema kupitia Al Jazeera kuwa uchaguzi ulitawaliwa na hotuba za chuki na vurugu. Akasema, hali ya upigaji kura kuanzia ufunguaji hadi ufungaji wa vituo ulikuwa salama, lakini alitoa tahadhari kwamba hali inaweza kubadilika ndani ya saa 72 kutokea Jumatatu.

Hofu kubwa ya wananchi wa Guinea ni siku matokeo yatakapotangazwa. Haionekani kama upo upande utaweza kukubali matokeo, ule wa Conde (chama tawala) au wa Diallo, unaoongoza upinzani.