Nyimbo za Bob Marley zinavyotumika kuhamasisha kampeni za Tundu Lissu

Muktasari:

Wimbo huo ndiyo umetawala katika kampeni za mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu kila anapohutubia wananchi katika mikutano yake kote anakopita.

One love, one heart, let’s get together and feel all right. One love one heart, give thanks and praise to the lord and I will feel all right.

Hicho ni kibwagizo cha wimbo One love ulioimbwa na mwanamuziki mashuhuri wa reggae, Robert Nesta Marley, maarufu kama Bob Marley uliomo ndani ya album ya Exodus ya mwaka 1977.

Wimbo huo ndiyo umetawala katika kampeni za mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu kila anapohutubia wananchi katika mikutano yake kote anakopita.

Wimbo huo hupigwa mwanzo na baada ya hotuba ya Lissu pale Chadema inapotumia muda huo kukusanya michango, maarufu kama ‘sadaka ya ukombozi’ na kuzua shangwe kwa wafuasi na mashabiki wa chama hicho.

Tofauti na vyama vingine wanavyotumia wasanii kutumbuiza na kuhamasisha wananchi katika mikutano ya kampeni, Chadema wamekuwa wakitumia nyimbo za Bob Marley kuhamasisha kampeni zao.

Wakati zinapigwa wafuasi na wapenzi wa chama hicho hujumuika kucheza, huku wakitoa michango kwenye vikapu mbele ya jukwaa na masanduku yanayotembezwa na watumishi wa chama katikati ya makundi ya watu mkutanoni hapo.

Mbali na kuwa msanii, Bob Marley pia alikuwa mwanaharakati wa siasa za ukombozi hasa kwa watu weusi, hivyo nyimbo zake nyingi zilizungumzia ukombozi kwa watu wanaonyanyaswa.

Ndiyo maana haikushangaza kumwona Bob Marley na kundi lake la The Wailers alipotua nchini Zimbabwe mwaka 1980 kutumbuiza kwenye sherehe za uhuru wa nchi hiyo, akiimba wimbo wa African Liberate Zimbabwe.

Wimbo wa One Love ulitungwa na kurekodiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1965 na kundi halisi la The Wailers ukiwa single, lakini mwaka 1977 Bob Marley na kundi lake walirekodi toleo jipya la wimbo huo na kuufanya kuingia katika chati za nyimbo bora nchini Uingereza.

Simulizi nyingine zinaonyesha kuwa wimbo huo ulitokana na tungo za wimbo wa People get ready (kuweni tayari) uliotungwa na Curtis Mayfield wa kundi la The Impression la Marekani mwaka 1958.

Ulipoimbwa kwa mara ya kwanza mwaka 1965, kundi la The Wailers halikutaja Mayfield kwa sababu sheria za Jamaica hazikulazimisha.

Lakini mwaka 1977 baada ya toleo jipya la wimbo huo kurekodiwa na studio ya Island Records, ulipewa jina la “One Love/People Get Ready” na walimtambua Mayfield kuwa sehemu ya utunzi wa wimbo huo kwa lengo la kuepuka sheria ya hakimiliki.

Bob Marley aliuimba wimbo huo kufuatia vurugu za uchaguzi mkuu wa Jamaica uliofanyika Desemba 1976 unaotambuliwa kuwa wenye vurugu zaidi katika historia ya nchi hiyo, ukiwahusisha mahasimu wawili, Michael Manley wa chama cha People’s National (PNP) na Edward Seaga wa Jamaican Labour Party (JLP).

Mwaka 1972, Bob Marley alimuunga mkono Manley katika kampeni zake na hatimaye akashinda na kuwa Waziri Mkuu wa Jamaica, lakini kipindi hicho, Marley alijiweka pembeni kwa kuamua kutokuwa na upande wowote.

Licha ya kutoungwa mkono na Marley, Manley alifanikiwa kutetea nafasi yake na kuendelea kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

Marley aliurejea wimbo huo kwa lengo la kuwaunganisha Wajamaica waliokuwa katika mvutano mkali wa siasa.

Wimbo mwingine wa Bob Marley unaopigwa kwenye kampeni za Lissu ni wa Get up stand up.

Wimbo huo ambao upo kwenye album ya Burnin, ulitungwa na Bob Marley na Peter Tosh walipokuwa na kundi la The Wailers mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Katika wimbo huo, walihamasishana kusimama kupinga ukandamizaji, huku pia wakitaka imani yao ya Rastafarian iheshimiwe nchini Jamaica.

Wimbo mwingine ni Africa Unite ambao pia hupigwa katika mikutano hiyo na kuwafanya wafuasi na mashabiki wa Chadema kucheza kwa pamoja.

Mbali na nyimbo hizo upi wa ‘Tundu Lissu wapeleke mchakamchaka’ uliotungwa na msanii ajulikanaye kwa jina la Mwingira, pia unaonekana kukonga nyoyo za wafuasi wa chama hicho.