Wakataeni wenye nia ya kudhoofisha amani ya nchi – RC Adam Malima

Muktasari:

Watanzania wametakiwa kuwakataa watu wenye nia ya kudhoofisha amani na utulivu wa nchi.

Musoma. Watanzania wametakiwa kuwakataa watu wenye nia ya kudhoofisha amani na utulivu wa nchi.

Akifungua kikao cha kamati ya Amani ya Mkoa wa Mara leo Alhamisi Oktoba 22, 2020, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema Watanzania wanapaswa kuepukana na watu wa namna hiyo badala yake washirikiane kulinda tunu hizo za Taifa hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Malima amesema amani na utulivu ni sifa na msingi mkuu wa Utanzania, hivyo hakuna sababu ya Watanzania kukubali kupoteza sifa na msingi huo muhimu kwa kukubali kufanikisha malengo ya watu wachache wenye nia ya kuivuruga nchi kwa maslahi yao binafsi.

“Zipo nyakati amani, utulivu na umoja vinaweza kutetereka katika jamii ama nyingi na nyakati hizi tulizonazo Watanzania ni miongoni mwa nyakati ambazo vitu hivyo vinaweza kutetereka kwa hiyo niwaombe watanzania kwa umoja wetu tushikamane na uchaguzi usitumike kama chanzo cha kutetereka kwa tunu hizi,” amesema Malima.

Pia, amewataka Watanzania kuvumiliana kwa maelezo kuwa uhuru wa kisiasa usitumike kuathiri maisha ya kila siku katika jamii na kwamba, kamwe watu wanaotafuta uongozi wasivuke mipaka hadi kufikia kuhatarisha amani ya nchi.

Akichangia hoja katika kikao hicho, Katibu wa Kamati ya Amani Musoma mjini, Juma Masirori amesema kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa ni chanzo cha kuteteresha amani katika jamii.

Amesema viongozi hao wanatumia uhuru wa kisiasa vibaya na kusababisha chuki kwa jamii bila sababu ya msingi huku akipendekeza viongozi hao wadhibitiwe na  vyombo husika mapema.