Mgaywa wa SAU aahidi kumpatia uwaziri mkuu Dk Magufuli akiingia madarakani

Muktasari:

Anasema Dk John Magufuli ni mchapakazi, anafaa kuwa waziri mkuu wake akiingia madarakani na ameona kuna mawaziri watatu wa Serikali ya CCM wanafaa kuteuliwa kuwa mawaziri.

Dodoma. Mgombea urais wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Muttamwega Mgaywa amewataka Mawaziri watatu wa serikali ya Rais John Magufuli kwamba hatawaacha pindi akiingia Ikulu.

Mbali na mawaziri hao lakini amemtaja Rais Magufuli kuwa akikubali atampa nafasi ya Waziri Mkuu kwa kuwa ameridhishwa na utendaji wake na kuwa aliyoyafanya siyo ya kubeza.

Muttamwega ametoa kauli hiyo leo Oktoba 25,2020 jioni Jijini Dodoma akiwa safarini kuelekea Mara ambako amesema ndiko anakokenda kumalizia kampeni zake akisubiri kupelekwa Ikulu.

Mgombea huyo amewataja mawaziri ambao wanauguza moyo wake katika utendaji ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Ummi Mwalimu (Afya) na Selemani Jafo (Tamisemi) ambao amesema atawateua katika serikali yake.

“Kama mwenzako amefanya kazi nzuri basi mpongeze, huyu Rais Magufuli amefanya kazi kubwa na nzuri ni muhimu kushukuru, lakini mimi nitaanzia hapo alipoishia na nitaleta ndege 30 katika Uongozi wangu,” amesema Mgaywa.

Akizungumzia kampeni zake amesema amezunguka nchi nzima na Watanzania wamemuelewa hivyo watamchagua yeye bila kujali viongozi waliokuwa wanajaza watu kwenye mikutano yao.

Amewaomba wagombea wenzake kukubaliana na matokeo kwa atakayechaguliwa kwamba waungane pamoja na kumpongeza kwani huyo amechaguliwa kwa sababu watu wamemuamini kinachotakiwa ni kumpa mkono na kumtakia Uongozi mwema.

Mgombea huyo amesema katika Uongozi wanamtafuta mtu atakayeleta maendeleo nchini akiwemo yeye ambaye anakwenda kuunda Wizara 12.