Kusumbua kwa mtandao wa intaneti kunavyokwamisha biashara na maisha

Muktasari:

Mtandao ndio kila kitu katika maisha ya sasa. Wafanyabiashara na wajasiriamali wamehamisha shughuli zao mtandaoni. Hata maisha ya kijamii sasa yamo mitandaoni.

Dar es Salaam. Mtandao ndio kila kitu katika maisha ya sasa. Wafanyabiashara na wajasiriamali wamehamisha shughuli zao mtandaoni. Hata maisha ya kijamii sasa yamo mitandaoni.

Hata hivyo, watu wengi sasa wanalia baada ya mambo yao mengi kukwama kutokana na mtandao wa intaneti nchini kuanza kusumbua kwa zaidi ya wiki sasa.

Hali hiyo imekuja huku kukiwa hakuna mtoa huduma ya mtandao yeyote aliyetolea ufafanuzi jambo hilo. Jitihada za gazeti hili kupata ufafanuzi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hazikufanikiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, James Kilaba alipatikana lakini akasema hawezi kuzungumzia kwa kuwa yupo nje ya ofisi.

Kama ambavyo shida ya mtandao ilianza bila taarifa siku chache kabla ya siku ya kupiga kura (Oktoba 28, 2020), matarajio ya wengi yalikuwa ni kurejea kwa huduma hiyo mapema ili maisha yaendelee, lakini tatizo bado lipo.

Licha ya kuwa hakuna kampuni wala taasisi yoyote iliyoeleza kuwa imepata hasara itokanayo na tatizo la mtandao, Mwananchi linatambua kuwapo kwa kampuni zinazotoa huduma kwa njia ya intaneti ambazo mapato yamepungua kutokana na suala hilo.

Wafanyabiashara wadogo huweka picha za bidhaa zao mitandaoni na kutaja bei na chini yake huweka namba ya simu ili wanaohitaji wawapigie, lakini tatizo la mtandao kwa ambao hawakuwahi kupakua programu wezeshi hawawezi kutuma picha hizo.

Husana Hussein, ambaye ni muuzaji wa nguo na viatu kwa kutumia mitandao ya kijamii, aliliambia gazeti hili kuwa tatizo hilo ;omekwamisha shughuli zake na kumkosesha mapato.

Hussein alisema amekuwa akichuuza bidhaa zake kwa kuzitangaza kwenye mitandao ya Instagram, facebook na za WhatsApp.

“Lakini sasa watazamaji wamepungua kwa zaidi ya nusu. Wengi hawapo mtandaoni tena,” alisema Hussein.

Alisema mauzo ya biashara yake yanategemea zaidi watu wanaoziona bidhaa, lakini kwa sasa wengi hawawezi.

“Sasa hivi siuzi kama zamani maana bidhaa nyingi zilizopo katika kurasa zangu watu walishaziona. Sina uwezo wa kupakia bidhaa mpya kila mara. Lakini hata wanunuaji hakuna kwa kuwa watazamaji wamepotea,” alisema Hussein.

Abdul Latif, ambaye anauza bidhaa kutoka nje ya nchi zikiwamo saa za mkononi, alisema licha ya biashara yake kuathiriwa na kukosekana kwa intaneti, aliendelea kuwasiliana na wateja waliopakua programu wezeshi ya VPN.

“Ni kweli biashara imeathirika kwa sababu wateja wamepungua mtandaoni, lakini wapo wachache wanaotumia VPN. Tunaamini mtandao utarudi, tutaendelea na biashara,” alisema.

Athari ya shida ya mtandao wa intaneti haijaishia kwa watu ambao wanauza bidhaa zao katika mitandao ya kijamii, balihata huduma nyingine ambazo ambazo zinategemea intaneti.

Mkazi wa Kariakoo, Agnes Lameck alisema amekuwa akipata wakati mgumu kufuatitilia habari

‘‘Nilishaacha kununua magazeti na redio ni mara mojamoja. Sasa mtandao nao hakuna, nakosa habari kupitia simu yangu,’’ alisema.

Imezoeleka kuwa watumiaji wengi hununua vifurushi kwa ajili ya matumizi tofauti, lakini kwa hali iliyopo kuna uwezekano mkubwa kasi ya kununua ikawa imepungua.

Msemaji wa kampuni ya Uber Afrika Mashariki, inayotoa huduma ya usafiri wa abiria kwa kwa njia ya mtandao, Lorraine Onduru alisema kampuni hiyo inatambua hali inayoendelea hapa nchini na wanafanya juhudi kuhakikisha abiria na madereva wanaendelea kupata huduma kama kawaida.

Uber ina programu wezeshi ambayo humuwezesha mtu anayetaka huduma ya usafiri kujulikana yuko eneo gani na yeye kuona gari linalomfuata limefika wapi baada ya kuliomba kwa njia ya simu.

Oktoba 30 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilitoa tamko lake la kueleza masikitiko juu ya tatizo la hali ya kutopatikana kwa mitandao bila mamlaka husika kutoa taarifa ya sababu za tatizo hilo.

“Watumiaji wa mitandao wamelalamika kutoweza kutumia WhatsApp, Instagram, Twitter na YouTube na kujikuta wakikosa haki yao ya msingi ya kupata taarifa. Kumekuwepo na taarifa za baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuendelea kutumia mitandao hiyo kwa kupitia teknolojia ya Virtual Private Network (VPN) ambayo si rafiki na iliyozoeleka,” alisema mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga.

Aidha, LHRC walitoa wito kwa TCRA kutoa ufafanuzi wa hali ya kutopatikana kwa mitandao kwa sehemu kubwa ya watumiaji wa mitandao hiyo.

Pia, iliiomba kuchukua hatua za makusudi ili kurejea hali ya awali kwa kuwa mitandao ya kijamii imekuwa na msaada katika shughuli za kijamii na kiuchumi.