Ndugai: Wabunge msiwe mabubu,timizeni wajibu wenu

Ndugai: Wabunge msiwe mabubu,timizeni wajibu wenu

Muktasari:

Spika wa Bunge la 12,  Job Ndugai amewaasa wabunge wasiwe bubu badala yake watimize wajibu wao.

 

Dodoma.  Spika wa Bunge la 12,  Job Ndugai amewaasa wabunge wasiwe bubu badala yake watimize wajibu wao.

Ndugai amesema hayo leo Jumanne  Novemba 10, 2029 muda mfupi baada ya kuapa kuwa Spika wa Bunge.

Amesema ndani ya Bunge ndiyo kunapelekwa bajeti ya Serikali, kunatungwa sheria na mipango ya Serikali, hivyo ni vema wabunge wakatimiza wajibu wao.

"Ukichagua kuwa mbunge bubu, unajipendekeza ili uonekane una nidhamu, umeliwa, " amesema Ndugai.

Amesema siyo vema kwa mbunge kujipendekeza ili aonekane ana nidhamu kwenye chama au Serikali hatokuwa ametimiza wajibu wake wa kuwasemea wapiga kura wake.

Ndugai amesema wabunge watimize wajibu wao wa kuisimamia Serikali  kwa kuhakikisha zinatungwa sheria bora kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Pia, amesema lazima wabunge waonekane kwenye vyombo vya habari kwamba wanaisimamia Serikali vizuri.

Ndugai amesema kwa kuwa Bunge la 12 lina wabunge wengi wa CCM, hivyo kujifungia bila kuonekana kwa wananchi kupitia vyombo vya habari watahukumiwa mapema kwamba wapo kwa ajili ya kupendelea chama tawala.

Amesema miongoni mwa wabunge watateuliwa kuwa mawaziri, hivyo wafahamu lazima wafanye kazi na hakuna kubebana.

Pia, amesema wabunge wote wana haki ikiwamo wale wachache wa upinzani.

Ndugai amewatahadharisha wabunge kuacha kukopeshana fedha kwa kuwa katika Bunge la 11 walipata kazi kutokana na kesi za kudaiana.

"Nasema mapema mkikopeshana iwe huko huko, mimi sihusiki, " amesema Ndugai.

Baada ya Ndugai kutoa wosia huo wabunge walianza kuapa.