Wakazi 2,868 kulipwa Sh7 bilioni kupisha mradi wa maji mkoani Dodoma

Thursday October 10 2019Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Wakazi 2,868 wa vijiji vya Bubutole na Mwambose Wilaya ya Chemba nchini Tanzania Oktoba 15, 2019 wataanza kulipwa fidia kupisha ujenzi wa mradi wa maji bwawa la Farkwa.

Mradi huo utapeleka maji katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Dodoma Mjini, Bahi, Chemba na Kondoa.

Sh7 bilioni zimetolewa na Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya ulipaji fidia kwa wakazi hao.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Oktoba 10,  2019 mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amesema ulipaji fidia utaanza Oktoba 15 hadi 31, 2019.

“Fedha hizi ziko wizarani (Wizara ya Maji ) kuanzia Agosti mwaka huu. Fidia itahusisha mali zote za wananchi na taasisi mbalimbali ambazo ni makanisa, misikiti, ofisi za vijiji na za vyama vya siasa,” amesema.

Odunga amesema fidia hiyo haitahusisha fidia kwa taasisi za Serikali ikiwemo shule, zahanati na miradi mbalimbali.

Advertisement

Amesema ili kurahisisha zoezi hilo la ulipaji wa fidia Katibu Mkuu Wizara ya Maji ameunda kikosi maalum na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kikosi hicho.

Amesema kisheria wakazi hao wanapewa siku 90 kuhama katika eneo husika mara baada ya kupokea malipo yao.

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia amewataka kutumia fedha hizo kwa ajili ya maendeleo yao.

“Wakimama hakikisheni mnashirikiana bega kwa bega na wanaume wenu ili kutoleta migogoro ya kifamilia hasa ndoa kuvunjika kwa ajili ya ufujaji wa pesa,” amesema.

 

Advertisement