29 wapandishwa kortini Morogoro tuhuma za uzembe, uzururaji

Muktasari:

  • Polisi wamefanya shughuli ya kuwakamata wazururaji na wazembe ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo viovu na kuwafikisha mahakama ya Nunge Manispaa ya Morogoro.

Morogoro.  Watu 29 wakiwemo wasichana na wavulana wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Nunge Manispaa ya Morogoro nchini Tanzania kwa kosa la uzembe na uzururaji.

 hata nje ya mahakama washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na biashara ya ngono.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Emelia Mwambagi imedaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao ambao wengi wana umri chini ya miaka 20 walitenda kosa hilo Agosti 16, 2019 saa 6 usiku eneo la Kahumba wakiwa wanazurura bila ya kuwa na kazi yoyote.

Imedaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao wote kwa pamoja walikamatwa na askari polisi mwenye namba F3214 D/Cpl Anord Njiro aliyekuwa doria na wenzake katika eneo hilo la Kahumba.

Baada ya kusomewa shtaka hilo washtakiwa wote wamekana hata hivyo upande wa mashtaka umedai kuwa una mashahidi wawili kwa ajili ya kuthibitisha shtaka hilo.

Hakimu Mwambagi ameieleza Mahakama kuwa washtakiwa hao wanayo haki ya kupata dhamana kama watatimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja kwa kila mshtakiwa atakayesaini hati ya dhamana ya Sh.1 milioni.

Sharti jingine kila mshtakiwa ametakiwa kuwa na mdhamini mwenye kitambulisho cha taifa, kitambulisho cha kupigia kura na barua ya mwenyekiti wa mtaa na ofisa mtendaji wa kata.

Wakati kesi hiyo ikiendelea kusomwa mahakamani hapo washtakiwa hao walionekana kuinamia chini huku wengine wakificha nyuso zao kwa kanga hasa kutokana na kile kinachodaiwa kuwa washtakiwa hao wanajihusisha na vitendo vya biashara ya ngono.

Taratibu za dhamana zinaendelea huku kesi hiyo ikiahirishwa hadio keshp Jumanne Agosti 20,2019 ambapo ushahidi utatolewaa na mahakama itatoa hukumu.