5G ya Huawei kupenya soko la Uingereza

Muktasari:

Huawei inakadiriwa kuchangia mapato ya ndani ya Uingereza kwa takribani paundi 1.7 bilioni kwa mwaka 2018 , kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya tafiti za kiuchumi ‘Oxford.

Dar es Salaam.  Katika safari ya kufanikisha usambazaji huduma za mtandao wa Intaneti wa 5G, Kampuni ya Huawei inayozalisha vifaa mbalimbali vya kieletroniki zikiwamo simu zenye mfumo wa Android, imefanikiwa kupenyeza soko lake nchini Uingereza kwa ajili ya miundombinu ya mawasiliano.

 Hatua hiyo inachagizwa na tukio la Januari 28, mwaka huu baada ya Serikali ya Uingereza kukubaliana na Huawei kusambaza mtandao huo wenye kasi zaidi. Makubaliano hayo yalifanyika kupitia mkutano wa baraza la usalama nchini humo chini ya mwenyekiti wake ambaye ni Waziri Mkuu, Boris Johnson.  

 Mtandao wa intaneti wa 5G ni mwendelezo wa tano wa utumiaji wa mifumo ya simu bila kuunganisha na waya wakati wa mawasiliano ya simu na vifaa vingine kwa matumizi ya ofisini na nyumbani.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma mapema wiki hii, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Huawei, Victor Zhang amesema Serikali ya Uingereza imeihakikishia Huawei kuendelea kufanya kazi na wateja wake kupitia mfumo wa 5G.

 “Uamuzi huo utasaidia kuleta matokeo makubwa yenye usalama, ufanisi na kwa gharama nafuu katika huduma za miundombinu ya mawasiliano ya simu  yanayohitajika kwa maendeleo ya baadaye na itasaidia Uingereza kuifikia dunia yote kupitia teknolojia na kujihakikishia ushindani mkubwa,” amesema Zhang.

 Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali ya Uingereza itaruhusu huduma hiyo kwa makusudi ya kuijenga  Huawei kuchochea ukuaji wa teknolojia kwa kizazi kijacho licha ya hofu iliyotolewa na Marekani kwamba ikiruhusiwa huduma hiyo itaathiri shughuli za kibiashara nchini humo.

 Hata hivyo, Huawei inakadiriwa kuchangia mapato ya ndani ya Uingereza kwa takribani paundi 1.7 bilioni kwa mwaka 2018 , kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya tafiti za kiuchumi ‘Oxford.