ACT- Wazalendo kuzifuta kesi za kisiasa, kuboresha mazingira ya biashara

Muktasari:

Tanzania itafanya uchaguzi mkuu Oktoba 2020 ambapo Chama cha ACT- Wazalendo kimesema kikipata ridhaa ya kuongoza dola itahakikisha inazifuta kesi za kisiasa na kuweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha siasa cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kikipata fursa ya kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 watafuta kesi zote za kisiasa.

Pia, amesema watazifuta kesi za watu waliobambikiziwa na kuwalipa fidia waliolipishwa fedha mahakamani.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Machi 14, 2020 katika mkutano wa pili wa mwaka wa chama hicho unaofanyika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam unaokwenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Zitto amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani na wafanyabiashara wamekuwa wakibambikiwa kesi bila ya kuwa na makosa yoyote huku wengine wakilipishwa fedha.

“Kwanza tutapambana na rushwa na kuondoa vikwazo walivyowekewa watu wote walioonewa katika kipindi cha miaka minne kwa kubambikiwa kesi ili kuhakikisha kwanza wanaachiwa huru.”

“Kwa wale waliohukumiwa adhabu mbalimbali kwa uonevu watafutiwa rekodi za adhabu zao na kurudishiwa fedha walizotozwa kwa sababu hiyo ni ndoto ya ACT- Wazalendo,” amesema

Kwa upande wa wafanyabiashara, amesema wamelenga kuwawekea mazingira mazuri ya ufanyaji biashara halali lakini pia kuhakikisha mnalipa kodi zenu na kutonyonya wafanyakazi wenu.

Amesema kufanya hivyo kutawapa motisha ya kuzalisha zaidi ili kuongeza ajira na kupanua pato la taifa.

“Nasema hivyo kwa sababu katika kipindi cha miaka mitano ya CCM imewaacha hiloi kwa kuwabambikia makodi makubwa na kuwafunga jela na wengi wenu kukimbia nchi,” amesema Zitto