ACT- Wazalendo wajitoa kushiriki uchaguzi Serikali za mitaa

Friday November 8 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania kimetangaza kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Kamati ya uongozi ya chama hicho imewaagiza wagombea wake 173,593 kutoshiriki uchaguzi huo.

Kati ya wagombea 173,573 waliochukua fomu za uteuzi na kurejesha, wagombea 6,944 ndio waliopitishwa sawa na asilimia nne huku 166,649 wakienguliwa.

Uamuzi wa ACT- Wazalendo umekuja ikiwa imepita siku moja tangu Chadema kutangaza kujitoa kushiriki uchaguzi huo kutokana na figisufigisu zilizofanyika katika uchukuaji, urejeshaji wa fomu za kugombea na uteuzi wa wagombea.

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 8, 2019 kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe amesema  sababu kubwa ya kutoshiriki ni namna wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi walivyowaengua wagombea wa chama hicho.

 “Asimilia 94 ya wagombea wetu wameenguliwa na wamebaki asilimia 4, maana yake watawala ndio wametususa sisi, wametuondoa katika uchaguzi. Katika mazingira kama haya chama kimeamua hawa waliobaki wajiondoe.”

Advertisement

“ACT- Wazalendo haitakuwa na mgombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa sababu asilimia 96 wameondolewa na wasimamizi wa uchaguzi,” amesema Zitto.

 

 

Advertisement