ACT Wazalendo kukata rufaa hukumu ya Baba Levo

Wednesday September 11 2019

 

By Anthony Kayanda, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Chama cha ACT Wazalendo kimesema kinakusudia kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja jela alichopewa diwani wake wa Mwanga Kaskazini katika manispaa ya Kigoma Ujiji, Clayton Chipando maarufu Baba Levo.

Diwani huyo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na mahakama ya wilaya Kigoma jana Jumanne Septemba 10, 2019 baada ya kushindwa rufaa yake aliyokata kupinga hukumu ya kifungo cha miezi mitano jela aliyopewa awali na mahakama ya mwanzo Mwandiga Agosti 01, 2019.

Katibu wa ACT Wazalendo mkoa wa Kigoma, Juma Ramadhani ameiambia Mwananchi leo Jumatano Septemba 11, 2019 kwamba licha ya mshituko waliopata, chama hicho kitakaa na wanasheria wake ili kuona namna ya kukata rufaa au ikibidi kuachana na suala hilo.

"Chama hakijakata tamaa licha ya mahakama ya wilaya (Kigoma) kuamua kufanya uamuzi wake wa kupinga rufaa ya diwani wetu, bado kuna ngazi nyingine za juu na tutaona kama ipo haja ya kutafuta haki ngazi za juu au la tusubiri nyakati nyingine ikibidi," amesema Ramadhani.

Hukumu hiyo ya Baba Levo kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela imezima ndoto za msanii huyo wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania kugombea udiwani katika uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Mwailwa Pangani ameliambia Mwananchi kwamba amepokea taarifa ya diwani huyo kuhukumiwa kifungo hicho jela, hivyo anasubiri nakala ya hukumu ili wajue hatua nyingine zaidi za kiuongozi.

Advertisement

Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussen Ruhava ambaye anatokana na chama cha ACT Wazalendo amesema walikata rufaa kutokana na uzito wa hoja walizokuwa nazo lakini mahakama imezitupilia mbali.

Awali, Agosti 01, 2019 Baba Levo alihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela na mahakama ya mwanzo Mwandiga  kwa kosa la shambulio kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani, F.8350 PC Msafiri Mponela.

SOMA ZAIDI

Advertisement