ACT-Wazalendo wadai Maalim Seif bado anashikiliwa

Maalim Seif Sharif Hamad

Muktasari:

Chama cha ACT-Wazalendo kimedai mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad bado anashirikiwa na polisi.

Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimedai mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad bado anashirikiwa na polisi.

Maalim Seif alikamatwa leo mchana Alhamisi Oktoba 29, 2020 wakati akijiandaa kwenda eneo la mzunguko wa Michenzani kwa ajili ya maandamano muda mfupi baada ya kuzungumza na wanahabari kuhusu mwenendo wa uchaguzi akisema hajaridhishwa na mchakato wake.

Hata hivyo, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohammed Haji Hassan alipotafutwa na Mwananchi Digital leo jioni kuzungumzia kushikiliwa kwa Maalim amesema, “bado tunaendelea na hatua za uchunguzi ni mapema  kutoa taarifa.”

Katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano kwa umma wa chama hicho, Salim Bimani amesema mbali na Maalim Seif wengine waliokamatwa ni makamu mwenyekiti wa ACT Zanzibar,  Juma Duni Haji; Mohammed Nuru Mohammed na Ismail Jussa (wote wajumbe wa kamati kuu).

Bimani amedai kwa Jussa yupo hospitali akipatiwa matibabu baada ya kuvunjika mguu na mkono wakati wa purukushani zilizotokea  mchana maeneo ya Darajani.

"Bado  Maalim Seif  na wenzake  hawajaachiwa na polisi nadhani leo atalala rumande," amesema Bimani.