ACT-Wazalendo wasema Zitto Kabwe ataripoti polisi kwa wito maalum

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Muktasari:

  • Wakati Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni nchini Tanzania likisisitiza kumuhitaji kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kwa ajili ya kumhoji, chama hicho kimesema kiongozi wao huyo hawezi kuitikia wito huo kwa kuwa si rasmi.

Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni nchini Tanzania likisisitiza kumuhitaji kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kwa ajili ya kumhoji, chama hicho kimesema kiongozi wao huyo hawezi kuitikia wito huo kwa kuwa si rasmi.

ACT Wazalendo kimesema ili Zitto aripoti polisi ni lazima atumiwe wito maalum  unaotambulika na si kupitia vyombo vya habari.

Jana Ijumaa Agosti 17, 2019 kamanda wa polisi wilayani humo, Mussa Taibu alilieleza Mwananchi kuwa Zitto anatakiwa kufika kituoni kwa mahojiano.

Alitoa kauli hiyo baada ya polisi kuzuia mkutano wa mbunge huyo wa Kigoma Mjini na waandishi wa habari ulikuwa ufanyike katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Zitto alipanga kuzungumzia mkutano wa 39 wa wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) unaoendelea nchini.

Licha ya Zitto kutopatikana Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema, “Zitto hajapokea wito maalum wa kuitwa, RPC ametoa wito wa kisiasa. Na wakifanya hivyo Zitto atakwenda kuitikia wito huo lakini kama ni hivi (kupitia vyombo vya habari) hawezi kwenda.”

Leo Taibu amesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yupo katika mkutano wa Sdc, “Nipo kwenye masuala ya Sadc huku na masuala hayo ni kituoni.”