ACT Wazalendo yaishauri Serikali ya Tanzania mambo matano kuhusu corona

Muktasari:

  • Chama cha siasa cha upinzani nchini Tanzania cha ACT- Wazalendo, ameitaka Serikali kuchukua hatua za hatua za haraka ikiwa pamoja na kuzuia watu wanaingia kutoka nchi zenye maambukizi.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania, kimeishauri Serikali mambo matano ya kukabiliana na maambukizi ha ugonjwa wa corona ikiwa pamoja na kudhibiti watu wanaoingia kutoka nchi zenye maambukizi.

Katika tamko lililotolewa na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe leo Ijumaa Machi 20,2020 chama hicho kimetaka pia watu waliopita nchi za maambukizi kupimwa vya kutosha.

“Kuzuia safari za kwenda au kuingia nchini za watu kutoka nchi zilizoathirika zaidi na virusi vya corona, nchi hizo ni China, Italia, Iran, Uhispania, Ujerumani, Uingereza, Canada, Marekani, pamoja na nchi yoyote ambayo itaonekana kuwa na maambukizi zaidi,” amesema Zitto.

 “Kuwahimiza watu wote waliosafiri kutoka kwenye nchi zenye maambukizi zaidi ya vizuri vya corona ndani ya wiki tatu zilizopita kujitokeza na kufanyiwa vipimo kubaini kama wana maambukizi ama la.”

Pia, Zitto ameishauri Serikali ya Tanzania kununua chakula cha dharura cha kuhimili zaidi ya mwezi mmoja kutoka kipindi cha siku tatu cha sasa.

“Chakula husika kihifadhiwe na kugaiwa bure ama kwa bei nafuu mno pale athari za janga la corona litakapozidi na kuathiri hali ya chakula nchini.

“Serikali ina wajibu wa kueleza hatua inazochukua kuhakikisha hakuna uhaba wa bidhaa za mafuta ya kula na sukari (ya matumizi ya kawaida na ile ya viwandani),” amesema mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo)

Pia, ameitaka Serikali kurudisha fedha za wamiliki wa viwanda zitokanazo na kodi za ongezeko la thamani (VAT) za uagizaji wa sukari viwandani akisema wenye viwanda wamekuwa wakizidai kwa miaka minne sasa.

“Bunge la Bajeti lijadili tathmini ya hali ya chakula na uzalishaji wa bidhaa za chakula nchini, lipitishe fedha za dharura za ununuzi wa chakula cha akiba, pamoja na kupitisha unafuu wa kikodi kwa waagizaji wa chakula na bidhaa kutoka nje katika kipindi hiki cha dharura,” amesema Zitto