ADC watoa neno uchaguzi Serikali za mitaa, waitaja CCM

Muktasari:

Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema licha ya baadhi ya wagombea wake kuenguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kitashiriki uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Dar es Salaam. Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema licha ya baadhi ya wagombea wake kuenguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kitashiriki uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi  Novemba 16, 2019 na katibu mkuu wa chama hicho, Hassan Doyo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Doyo amesema licha ya kusimamisha wagombea zaidi ya 500 katika maeneo tofauti ni 216 pekee ndio waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo.

Wakati ADC wakieleza hayo vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, UPDP, NLD, Chauma, ACT-Wazalendo na CUF vimeshatangaza kutoshiriki uchaguzi huo kwa madai ya kutotendewa haki ikiwa ni pamoja na wagombea wake wengi kuenguliwa.

“Sisi ni mabingwa wa changamoto hatupelekwi na mihemko ya watu, tunapelekwa na misingi ya chama cha siasa kwa sababu  hata walipofuta matokeo ya uchaguzi Zanzibar wengine walisusa lakini sisi hatukufanya hivyo,” amesema Doyo

Doyo alitumia mkutano huo kumjibu katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliyedai kuwa wagombea wa upinzani walioenguliwa katika uchaguzi huo hawajui kusoma na kuandika.

“Anaposema walioenguliwa hawajui kusoma na kuandika maana yake analiingiza Taifa katika aibu kubwa ndani na nje ya nchi kwamba bado wajinga wapo, kwamba nchi hadi leo ina watu wasiojua kusoma na kuandika,” amesema Doyo.

Kampeni za uchaguzi huo zinaanza kesho Jumapili Novemba 17 hadi  23, 2019.