Abiria 50,579 wamesafiri na treni Dar- Moshi

Abiria 50,579 wamesafiri na treni Dar- Moshi

Muktasari:

Nauli inayotumika katika treni ni ndogo na mtu anaweza kubaki na akiba tofauti na angetumia usafiri mwingine.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania(TRC), Masanja Kadogosa amesema zaidi ya abiria 50,579 wamesafirishwa kupitia treni inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam kwenda Arusha kupitia Moshi na Tanga.

Pia, tani zaidi ya 26,000 za mbolea na saruji zimesafirishwa katika kipindi cha miezi 9 tangu treni hiyo ilipoanza safari kwenda Moshi kabla ya kufika Arusha.

Kadogosa amesema hayo katika uzinduzi rasmi wa treni ya abiria inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Arusha kupitia Moshi na Tanga iliyokuwa imeacha kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 30.

Amesema kabla ya uzinduzi huo, ulifanyika ukarabati uliogharamu zaidi ya Sh14 bilioni pesa zilizotolewa na Serikali huku kazi hiyo ikifanywa na wahandisi kutoka shirika la reli na kuajiri zaidi ya vijana 600.

“Kwa idadi ya hii ya abiria tuliowahudumia maana yake ni kuwa kuna Watanzania zaidi ya 5,000 wanaokuja Arusha, Moshi na Tanga wanategemea reli hii kwa sasa na tuna zaidi ya tani 2600 zinasafirishwa kila mwezi,” amesema.

“Nauli inayotumika katika treni ni ndogo na mtu anaweza kubaki na akiba tofauti na angetumia usafiri mwingine, kwa wafanyabiashara wadogo ina faida kwa sababu kabla hatujaanza tani moja ya mbolea walikuwa wanasafirisha kati ya Sh93,334 hadi Sh100,000 na sasa ni Sh46,000 tu kwa tani,”amesema Kadogosa.

“Maana yake ni neema kwa wakulima wa maeneo haya, kwa upande wa saruji walikuwa wanasafisha tani moja kwa Sh100,000 hadi Sh110,000 baada ya sisi kuja tani moja ni Sh68,000 unaweza kuona faida hii kubwa iliyoletwa na ujio wa reli,”amesema.

Amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wamepanga kuwa na miundombinu baridi kwa ajili ya wakulima wa maua na mbogamboga

“Tunataka kujenga hapa ili waweze kuhifadhi na kwa upande wa Dar es Salaam itakuwa eneo la Kurasini na hi itasaidia sana wakulima wa Mbogamboga,” amesema Kadogosa.