Abiria wachache wasitisha safari za mabasi Dodoma kuelekea Morogoro, Dar es Salaam

Stendi kuu ya mabasi yaendayo Mikoani Dodoma

Muktasari:

Baadhi ya magari katika stendi kuu mabasi Dodoma yanayofanya safari zake kupitia mkoani Morogoro   yameshindwa kusafirisha abiria akihofia kupata hasara baada ya abiria wengi kuahirishwa safari

Dodoma. Baadhi ya mabasi ya abiria katika stendi kuu ya mabasi Dodoma yanayofanya safari kupitia mkoani Morogoro yameshindwa kufanya safari leo Jumanne, Machi 3, 2020 baada ya kukokosa abiria.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukatika kwa daraja katika barabara kuu ya Dodoma-Morogoro eneo la Dumila mkoani Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi leo, Katibu wa Mawakala wa Mabasi Stendi Kuu Dodoma (Ummdom), Yahaya Iddi  amesema magari hayo hayajafanya safari leo kutokana abiria wengi kuahirishwa safari.
Iddi amesema mabasi hayo yaliahirishwa safari kwa kupitia kupata hasara kwa kupitia barabara ya mkoa wa Iringa-Morogoro baada ya kuona abiria walikuwepo ni wachache baada ya wengi kuahirisha safari.
"Mabasi yanayotokea hapa stendi kuu hayajafanya safari leo, abiria walikuwa wachache na walivyokuja hapa wamewaambia hali ilivyo wapo baadhi waliamua kurudi nyumbani na wengi wanatumia magari yanayotokea Singida, Tabora au mikoa ya Kanda ya Ziwa,"alisema Yahaya.
Hata hivyo, amesema magari ya kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa jana yalilala jijini Dodoma na leo asubuhi yaliendelea na safari kwa kupitia mkoani Iringa.
Alisema yale yenye vituo maalumu katikati ya jijini la Dodoma yameendelea na safari kama kawaida kwa barabara ya Iringa, Morogoro badala ya Dodoma Morogoro.
Mmoja wa abiria anayeenda Dar es Salaam, Joyce Geremia amesema alifika stendi tangu asubuhi lakini hajafanikiwa kupata usafiri.
Amesema alichoambiwa ni kusubiria magari yanayotoka mikoa ya Singida au Tabora kwa gharama ya Sh35,000 badala ya Sh20,000.