VIDEO: Abiria wafurahia usafiri wa treni Moshi- Dar

Muktasari:

Abiria wengi wa treni kutoka Moshi kwenda Dar es Salaam wameeleza jinsi usafiri huo uliorejea baada ya kupita miaka 25 ulivyo nafuu, hasa kwa wenye kipato cha chini. Mara ya mwisho treni hiyo kufanya safari kati ya Dar es Salaam - Moshi ilikuwa mwaka 1994.

Dar es Salaam. Ijumaa Desemba 6, 2019 treni ya abiria itakayokuwa ikitoa huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Moshi, mkoani Kilimanjaro ilirejea baada ya kupita  miaka 25.

Treni hiyo yenye mabehewa manane iliondoka Dar es Salaam  Ijumaa saa 10 jioni ikiwa na abiria 263 na 24 walipandia njiani.

Ilifika Moshi jana saa 5:30 asubuhi na siku hiyo saa 10 jioni ilianza safari kwenda Dar es Salaam na kufika leo Jumapili Desemba 8, 2019 saa 4:20 asubuhi. Iliondoka Moshi na abiria 241.

Teddy Momburi, mmoja wa abiria wa treni hiyo amesema, “nimefika salama na huduma ni nzuri na za uhakika, pia treni  ni safi.”

“Nauli ni rahisi ambayo ni Sh39,000, Sh23,500 na Sh19,000 kila mtu anaweza kumudu huu usafiri.”

Ramadhani Shomary amesema, “treni ipo vizuri, nimevutiwa na huduma zake. Ni mara ya kwanza napanda treni kutoka Moshi ingawa nimewahi kupanda treni kwenda maeneo mengine.”

Jamila Mustafa amesema, “nimependa usalama si kama basi. Pia ukiwa na watoto ni nzuri zaidi maana wanakaa vizuri wanaweza hata kucheza, kulala, kukaa. Mizigo pia unapanda nayo mingi zaidi si kama kwenye basi. Kwa kweli ni usafiri salama zaidi.”