Abiria wanusurika basi likiteketea kwa moto Kondoa

Muktasari:

Basi la abiria la kampuni ya Machame limeteketea kwa moto, lakini abiria waliokuwamo wamenusurika kufa, huku mmoja akivunjika mguu aliporuka kupitia dirishani.

Dodoma. Basi la abiria la kampuni ya Machame limeteketea kwa moto, lakini abiria waliokuwamo wamenusurika kufa, huku mmoja akivunjika mguu aliporuka kupitia dirishani.

Basi hilo lilitoka Arusha saa 12 asubuhi na lilikuwa likielekea Dodoma, huku abiria wakisema ni moja ya magari mapya katika kampuni hiyo.

Mashuhuda wa ajali hiyo wameeleza kuwa tukio hilo limetokea leo Oktoba 20,2020 saa tano asubuhi katika Kijiji cha Kolo wilayani Kondoa.

Mmoja wa abiria waliokuwa ndani ya basi hilo, Onesmo Mroki amesema ajali hiyo ilitokea mita chache wakati basi likitoka kituo cha Kolo.

Mroki amesema basi hilo lilisimama kushusha abiria kituoni hapo, lakini wakati linaondoka ndipo lilianza kutoa moshi kwa wingi na kuanza kuungua.

"Mimi mwenyewe ni dereva wa halmashauri, ninachoweza kusema sababu za kuungua zimetokana na mfumo wa umeme, lakini gari ni jipya na halikuwa na shida," amesema Mroki.

Kwa mujibu wa abiria huyo, mizigo iliyokuwa ndani ya gari hilo iliteketea yote kwa moto hasa iliyokuwa chini ya buti la gari.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto amesema hajapata taarifa za kuteketea kwa gari hilo na kuahidi kufuatilia ili atoe taarifa sahihi.