Afariki kwa kupigwa na radi akiendesha pikipiki

Muktasari:

Paul Chundu (27) mkazi wa mtaa wa Msasani manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi amepigwa radi na kufariki dunia wakati akiendesha pikipiki.

Katavi. Paul Chundu (27) mkazi wa mtaa wa Msasani manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi amepigwa radi na kufariki dunia wakati akiendesha pikipiki.

Tukio hilo limetokea juzi Machi 29, 2020 katika  mbuga ya Kalilankulukulu halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 31, 2020, Magret Maico ambaye ni mama mzazi wa Chundu amesema mwanaye alifariki dunia wakati akitoka kibaruani.

“Ijumaa nilikwenda naye shambani nikagundua kuna magugu, nilimshauri apeleke kibarua siku ya Jumatatu lakini alikataa na kutaka aende Jumapili  ili Jumatatu afanye shughuli nyingine,” amesema.

Amesema siku a tukio alichelewa kurudi nyumbani tofauti na ilivyozoeleka, na siku hiyo alipewa taarifa kwamba Chundu amefariki.

Mwenyekiti wa mtaa wa Msasani, Juvenary Deus amesema, “nimepokea taarifa hizi asubuhi baada ya kusikia kengele, sikuamini.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamini Kuzaga amethibitisha kifo hicho na kwamba mwili ulihifadhiwa hospitali ya rufaa ya Mkoa kwa uchunguzi.

"Mwili ulifanyiwa uchunguzi na baadaye tukawakabidhi ndugu kwa ajili ya maziko, marehemu ameacha mke na mtoto mmoja" amesema Kuzaga.

Hilo ni tukio la tatu kutokea Machi, 2020 baada ya watu wengine wawili kufariki kwa kupigwa na radi akiwemo mtoto wa miaka tisa.