Ahadi ya Rais Magufuli kwa vijana 2000 wa JKT yatimia, CDF Mabeyo atoa maelekeo

Muktasari:

Vijana 2033 walioshiriki ujenzi wa ukuta wa kuzunguka madini ya Tanzanite wilayani Mirerani mkoani Manyara  wametakiwa kufika kambi ya Jeshi Mgulani jijini Dar es Salaam kukamilisha taratibu za ajira ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo ametangaza neema ya ajira  kwa vijana wa kujitolea walioshiriki kikamilifu ujenzi wa ukuta wa Mirerani mkoani Manyara ambao hawakubahatika kuingia kwenye mchakato wa ajira.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 10,2019 na wanahabari jijini Dar es Salaam Jenerali Mabeyo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa Aprili 6,2018 wakati wa uzinduzi wa ukuta huo unaozunguka eneo ambalo madini ya Tazanite yanachimbwa.

Jenerali Mabeyo ameagiza vijana hao 2,033 kufika katika kambi ya Jeshi Mgulani keshokutwa Alhamisi Septemba 12, 2019 kwa ajili ya kuhakikiwa na kukamilisha taratibu za kuandikishwa ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Aidha amesema vijana hao wanatakiwa kuripoti wakiwa na cheti walichotunukiwa baada ya kumaliza ujenzi huo pamoja na cheti cha kumaliza mkataba wa mafuzno ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

“Vijana hao chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu wa wahandisi ujenzi ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, walitekeleza jukumu hilo kwa weledi, maadili na ufanisi.”

“Hata hivyo, kutokana na mchakato kuchukua muda mrefu wapo ambao hawajaweza chukuliwa mpaka sasa na kutokana na hilo wamekuwa wakihangaika kuwasiliana na viongozi wa ngazi mbalimbali kujua hatima yao hadi kuhisi kuwa walipewa ahadi hewa,” amesema.