Aida Khenan alivyojiandikia historia jimbo la Nkasi Kaskazini

Muktasari:

Aida ambaye ni miongoni mwa wanawake 26 walioshinda kwenye majimbo 264, aliwashinda wenzake watatu akiwamo Ally Keissy wa CCM, mbunge aliyemaliza muda wake na ambaye alijizolea umaarufu kutokana na hoja zake katika Bunge la 11.

Saa 5:00 usiku wa Oktoba 29, mwaka huu, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Missana Kwangura alitangaza jina la Aida Khenan wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa mshindi wa jimbo hilo baada ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

Aida ambaye ni miongoni mwa wanawake 26 walioshinda kwenye majimbo 264, aliwashinda wenzake watatu akiwamo Ally Keissy wa CCM, mbunge aliyemaliza muda wake na ambaye alijizolea umaarufu kutokana na hoja zake katika Bunge la 11.

Jimbo hilo lenye kata 17 ni moja ya majimbo mawili ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa iliyoanzishwa mwaka 1983, likiwa na rekodi ya kupata uwakilishi wa viongozi wanaume bungeni tangu uchaguzi wa kwanza wa 1995 chini ya mfumo wa vyama vingi kabla ya Aida kuandika rekodi mpya.

Katika mahojiano na Mwananchi, lililotaka kufahamu ni kwa namna gani alifanikiwa kushinda jimbo hilo akiwa mbunge pekee wa Chadema huku vigogo wengine wakiangushwa katika majimbo mbalimbali, alisema;

“Tunamshukuru Mungu tumeshinda, lakini hata Nkasi ilikuwa na nguvu sana kuanzia kipindi cha kampeni. Kwa mfano nilikuwa ninashambuliwa kwa kauli za udhalilishaji wa kijinsia majukwaani, utanisikia mgombea mwingine anasema msimpatie kura huyu hajaolewa, sio kauli za kurudia kusema.

Iliniumiza sana kwa sababu hata historia inaonyesha, Mkoa wa Rukwa haujawahi kupata mbunge mwanamke tangu kuanzishwa kwa majimbo hayo. Lakini sikukata tamaa na nashukuru wananchi wakanielewa na kunichagua kama mbunge wa kwanza mwanamke.

Ushindi wangu unafungua milango sasa kwa wagombea wengine wanawake kwamba, tukipewa nafasi inaweza kuongeza idadi kubwa ya wanawake kuaminiwa zaidi. Kwa hiyo namuomba Mungu anisaidie nifanikiwe kufikia malengo niliyokusudia katika jimbo hili.

Mwandishi: Unadhani ni kwa nini jimbo hilo halikuwahi kumwamini mwanamke katika historia yake na ijitokeze kwa sasa?

Aida: Ni changamoto ya mila na desturi tu ndiyo ilitufanya tuwe nyuma. Jamii ilikuwa inaamini mwanamke hawezi kufikia malengo aliyokusudia. Lakini bado kulikuwa na dhana ya kwamba, huyu ni mwanamke tu, atafanya nini tukimpa uongozi? Bado ipo, lakini kupitia mimi inaweza kumalizika.

Ikumbukwe kabla ya kuwa mbunge nimekuwa mwenyekiti wa vijana wa chama mkoa, pia nimewahi kugombea nafasi ya mwenyekiti mkoa wa chama (Chadema). Kwa hiyo uzoefu huo ulinijengea ujasiri wa kuamini hata nafasi nyingine ninaweza.

Kilichosaidia zaidi hata nilipokuwa mbunge wa viti maalumu bunge la mwaka 2015, nilipigania mahitaji ya wananchi bila kuangalia itikadi yangu. Ndiyo maana nimepigiwa kura nyingi na wenye vyama na wasiokuwa na vyama.

Sababu nyingine ya ushindi wangu inachagizwa na dosari za mbunge aliyemaliza muda wake pamoja na kushambuliwa kijinsia.

Kwa ujumla, uzoefu, uwezo wa kujiamini, changamoto za jimbo na mabadiliko ya mtazamo kwenye jamii ndiyo sababu za ushindi wangu.

Wananchi wameniamini kwa hiyo ninatakiwa kubeba imani hiyo ili kuwaonyesha mwanamke anaweza kuleta mabadiliko ndani ya jimbo, inawezekana kasumba ya kutomwamini mwanamke ikapotea lakini nikifanya vibaya, ninaweza kufunga kabisa nafasi ya mwanamke ndani ya jamii yetu.

Mwandishi: Ni matatizo gani yanayowakabili wanawake ndani ya jimbo hilo na ungetamani kuyapatia kipaumbele bungeni?

Aida: Kipaumbele changu ndiyo kipaumbele cha wananchi wangu. Sitakwenda na mawazo binafsi lakini nimejiwekea malengo kwa mambo manne ambayo ni huduma za maji, afya, elimu na barabara.

Kuhusu upande wa changamoto za mwanamke, ninatamani kushughulikia maeneo mengi ambayo serikali haikufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa mfano, jimbo hilo ni kinara wa mimba za utotoni mkoani Rukwa. Pili, wanafunzi wa kike wanasoma umbali mrefu. Takribani asilimia 40 ya vijiji 49 hakuna shule za msingi.

Tatu, watoto wa kike wanafuata maji umbali mrefu kwa sababu ya changamoto ya maji. Asilimia 32 ya vijiji hivyo hakuna maji licha ya kuzungukwa na ziwa Tanganyika.

Tunafikiria kila kitongoji tuwe na kisima kirefu ndani ya miaka mitano ijayo.

Jambo la nne, ni changamoto ya huduma za afya, wajawazito wanatembea umbali mrefu kwenda kujifungua.

Kuna wastani wa asilimia 20 tu ya kata 17 ndiyo kuna vituo vya afya. Sera ya afya inataka kila kijiji kiwe na kituo cha afya lakini haijatekelezeka bado.

Kuna changamoto pia ya barabara Kata ya Korongwe na Mwamba. Pia, kata ya Mkinga na Kipili zinahitaji barabara ili kusaidia shughuli za mzunguko wa biashara ili kusaidia mapato kwa halmashauri yetu. Itapunguza adha kwa wajawazito ya kujifungulia barabarani kwa kushindwa kufika mapema kwenye vituo vya afya.

Jana (Jumatatu) niligeuka mkunga, nilimsaidia kujifungua njiani ikiwa ni mara ya pili, kilichotokea ni kwamba, huyo mama alikuwa anatokea kata ya Korongwe anakuja Namanyere, lakini alikwama njiani eneo la Kijiji cha Lyazumbi…. nikapigiwa simu nikaenda na gari akajifungua mtoto wa kiume na baadaye tukampeleka kituo cha afya Mkomolo, kilichopo Namanyere.

Mwandishi: Pamoja na kujitoa huko, uko tayari kupokea uamuzi tofauti wa chama utakaoathiri mipango yako ya kuwatumikia wananchi bungeni kwa mara ya kwanza?

Aida: Mpaka sasa sijapewa taarifa yoyote na chama kwamba nisiende bungeni au niende na ninaamini, Chadema ni taasisi ina utaratibu wake. Ninaamini chama kilipitisha jina langu jimboni ili nikashindane, sasa nimeshinda na niko tayari kwenda kutekeleza yale wananchi waliyonituma.

Mwandishi: Vipi kuhusu uhuru wako ndani ya Bunge hilo lenye asilimia zaidi ya 90 ya wabunge wa CCM wasiohalalishwa na chama chako?

Aida: Tukiwa ndani ya jengo nitajisikia mpweke kidogo kwa maisha niliyozoea miaka mitano iliyopita lakini kwa kuwa nilichaguliwa na wananchi wa Nkasi Kaskazini na siyo wengine, kifikra nitakuwa huru kabisa na salama kabisa nikitegemea ujasiri wa wapiga kura wangu. Naamini chama changu kitanipatia baraka zote kuwakilisha wananchi wa jimbo letu.

Mwandishi: Una ushauri gani unapojiandaa kuingia bungeni?

Aida: Ushauri wangu kwa wabunge wenzangu wa CCM ambao ni wengi, wenye mawazo mbadala tutakuwa wachache kwa hiyo ninashauri kusikiliza maoni ya wachache halafu wao wafanye maamuzi. Pili nitashirikiana na kuheshimu maoni ya wananchi wa jimbo langu bila kuangalia itikadi za kidini, vyama. Jambo la msingi ni kushirikiana kwa pamoja na wadau wa maendeleo ili kuleta maendeleo.