MAJANGA: Ajali sita za ndege zasababisha vifo 16 nchini

Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na maafisa wa usafiri wa ndege wakiupakia mwili Nelson Mabeyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo kwenye chopa kwa ajili ya kusafirisha kutoka Serengeti kuelekea Dar e Salaam juzi. Picha na Anthony Mayunga

Muktasari:

  •  Agosti 6 mwaka huu, abiria tisa walinusurika baada ya ndege ndogo waliyokuwa wakisafiria kupata ajali wakati ikiruka kisiwani Mafia. Agosti 3 mwaka huu, raia wawili wa Afrika Kusini walikufa baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kuan-guka katika kijiji cha Igungwa wilayani Sikonge Mkoa wa Tabora.
  • Novemba 15 mwaka 2017, ndege ya kampuni ya Coastal Aviation ilipata ajali katika eneo la Ngorongoro na kusababisha vifo vya watu 11 wakiwemo marubani wawili. Ilianguka wakati watalii wakiwa wanapiga picha eneo la kreta ya Imbakai ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
  • Oktoba 25 mwaka 2017, ndege nyingine ya kampuni ya Coastal Aviation ilianguka, eneo la Lobo katika hifadhi ya Serengeti na watu wawili kujeruhiwa. Ndege hiyo aina ya Cessna Grand Caravan ilianguka wakati ikipaa katika uwanja mdogo uliopo katika eneo hilo.
  • Oktoba 8, mwaka jana ajali nyingine ya ndege ilitokea wilayani Monduli, baada ya ndege ndogo aina ya Safari Air link-DH- Sal aina ya Cessna 206 kuanguka na kusababisha kifo cha abiria

Arusha/Dar. Matukio ya ndege ndogo kuanguka nchini yameongezeka miaka ya hivi karibuni baada ya nyingine kuanguka jana na kusababisha vifo vya watu wawili akiwemo Nelson Mabeyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo.

Tangu mwaka 2017 hadi jana mchana, zimetokea ajali sita za ndege na kusababisha vifo vya watu 16.

Nelson alikuwa rubani katika ndege ya kampuni ya Auric Air iliyoanguka katika uwanja mdogo wa ndege wa Seronera uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania.

Ndege hiyo ilianguka jana saa 1:30 asubuhi wakati ikipaa katika uwanja huo kwenda mkoani Arusha.

Nelson aliondoka na ndege hiyo juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi jana msimamizi wa kampuni ya Auric, Peter Kimaro alisema Nelson alifariki dunia katika ajali hiyo akiwa na Nelson Orutu ambaye ni rubani mwanafunzi.

“Baada ya kuhakiki na kuona ndege iko sawa na kuruhusiwa kuruka kwenda Gurument kuwachukua wageni kuwapeleka Kia (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro), walipoingia na kuondoka, mimi nikajua wako sawa,” alisema.

Alisema baada ya kuona ndege imeshika mwendo kisha ikapaa kidogo, badala ya kunyooka juu ikakata kona, “na mimi nikashangaa kuona vile kisha ikagonga choo cha uwanjani na kuanguka na wote walifia ndani ya ndege.”

Alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji waliwahi kuzima moto na miili ilihifadhiwa katika zahanati ya Soronera ikisubiri utaratibu mwingine. Jana jioni miili hiyo ilichukuliwa kwa nyakati tofauti, wakati wa Nelson uliletwa Dar es Salaam wa Orutu ulipelekwa Arusha.

Jana, wageni 14 waliokuwa wasafiri na ndege hiyo walitafutiwa usafiri mwingine huku Kimaro akisema “wageni hao walikuwa wa kampuni ya And Beyond Tanzania na sisi tulikodiwa kuwasafirisha, baada ya tukio (ajali) tukachukua hatua ya haraka maana wale walikuwa na ratiba yao.”

Akizungumza jana ofisa uchunguzi wa Mambo ya Anga wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Paul Kweka alisema kuanzia jana saa 10 jioni walianza uchunguzi wa ajali hiyo utakaochukua siku mbili hadi tatu.

“Nitashirikiana na ofisa wa uchunguzi mstaafu, John Nyamihula ambaye huwa tunamtumia yanapotokea majanga ya namna hii. Tutatafuta chanzo kwa kuangalia eneo,” alisema Kweka.

Mwananchi lilifika nyumbani kwa Mabeyo jana na kushuhudia maturubai yakifungwa huku ulinzi ukiimarishwa.

Rais John Magufuli jana alikwenda nyumbani kwa Mabeyo maeneo ya Msasani kumpa pole kwa msiba huo.