Ajali ya moto Morogoro, vifo vyafikia 100

Muktasari:

Majeruhi mmoja kati ya 16 waliokuwa aliyekuwa  amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam nchini Tanzania  katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) amefariki dunia jana usiku Jumanne Agosti 20,2019.


Dar es Salaam. Idadi ya waliofariki kutokana na ajali ya moto wa lori la mafuta ya petroli lililoanguka kisha kuwakama moto eneo la Msamvu mkoani Morogoro nchini Tanzania Agosti 10, 2019 imefikia 100.

Hii inatokana na majeruhi mwingine mmoja kufariki jana usiku Jumanne  wa Agosti 20, 2019 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.

Kifo hicho kimekuwa cha tatu kwa siku ya jana Jumanne ambapo hadi saa 10 jioni ya jana Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kabwe alisema majeruhi wawili kati ya 18 walikuwa wamefariki.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa MNH, Aminiel Aligaesha amewataja waliofariki ni Mazoya Sahani, Khasim Marjani na Ramadhani Magwila.

Amesema majeruhi waliobaki katika hospitali hiyo waliolazwa chumba cha uangalizi maalum (ICU) ni 13 na wawili wametolewa ICU na kulazwa wodi ya Sewahaji.

MNH tangu ilipotokea ajali hiyo ilipokea majeruhi 47 waliofikishwa hospitalini hapo kwa nyakati tofauti wakitokea Morogoro ili kupatiwa matibabu ambapo sasa wamebaki 15 na wengine kufariki dunia.