Ali Kiba, Harmonize wamjibu Diamond kuhusu tamasha la Wasafi

Wednesday October 30 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Saa chache baada ya msanii,  Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz kuwaalika Harmonize na Ali Kiba katika tamasha la Wasafi, wawili hao wameibuka na kumjibu.

Wakati Ali Kiba akimtaka Diamond kutomfuatilia akitumia neno “unikome”, Harmonize amesema hataki kuongea kuhusu jambo hilo.

Leo mchana Jumatano Oktoba 30, 2019 Diamond wakati akizungumzia tamasha hilo litakalofanyika Novemba 9, 2019  jijini Dar es Salaam alisema ana imani Harmonize atashiriki na kwamba amepeleka mwaliko kwa uongozi wa Ali Kiba, ili msanii huyo naye ashiriki tamasha hilo.

"Wenzetu (wasanii) Nigeria ndio maana wanaendelea kwenye muziki kwani kunapokuwa na matamasha kama haya wanaweka tofauti zao pembeni, kumkuta jukwaa moja Wizkid na Davido ambao walikuwa na bifu kwao ni jambo la kawaida.”

“Kwa nini tung’ang’anie bifu hata sehemu ambayo ni ya kutengeneza pesa na kutuleta Watanzania pamoja,” amesema Diamond katika mkutano wake huo na waandishi wa habari.

Baada ya Diamond kueleza hayo, Mwananchi lilimtafuta Ali Kiba kujua kama ataweza kushiriki katika tamasha hilo na msanii huyo alisema hawezi kulizungumzia suala hilo.

Advertisement

Baada ya muda Ali Kiba alimjibu Diamond kupitia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Instagram, “usiniletee mambo ya darasa la pili unaniibia penseli halafu unanisaidia kutafuta unikome.”

 “Mwanaume huwa anaongea mara moja tu sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unayonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatokuja mtu sasa tuishie hapo nakutakia tamasha njema.”

Wakati Ali Kiba akieleza hayo, Harmonize alipoulizwa na Mwananchi amesema, “achana na hayo mambo ya Diamond, tuongee mambo mengine.”

Advertisement