VIDEO: Ali Mufuruki katika sura mbili ndani ya ukumbi wa Julius Nyerere

Muktasari:

Novemba 12, 2019 Ali Mufuruki aliingia katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) akitembea huku akitabasamu lakini leo Jumanne Desemba 10, 2019 watu wamekusanyika katika ukumbi huo kumuaga. Mufuruki amefariki dunia hatunaye tena.


Dar es Salaam. Novemba 12, 2019 Ali Mufuruki aliingia katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) akitembea huku akitabasamu lakini leo Jumanne Desemba 10, 2019 watu wamekusanyika katika ukumbi huo kumuaga. Mufuruki amefariki dunia hatunaye tena.

Siku ya mwisho alifika katika ukumbi huo katika uzinduzi wa kitabu cha Rais mstaafu Benjamin Mkapa cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu), leo Mkapa amefika katika ukumbi wa JNICC kwenye msiba wa Mufuruki, mmoja wa walioshuhudia na kupongeza kitabu chake. Hakuna aijuaye kesho hakika binadamu tunapita hapa duniani.

Mwili wa Mufuruki aliyefariki dunia juzi alfajiri uliwasili nchini Tanzania jana jioni ukitokea Afrika Kusini, baada ya kuagwa leo  utazikwa katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Viongozi, wastaafu, wafanyabiashara na wananchi wamejitokeza katika ukumbi huo idadi ambayo inatafsiri  kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akigusa maisha ya wengi.

Mufuruki aliyesoma Shule ya Msingi Katerero mkoani Kagera nchini Tanzania anazikwa leo Jumanne katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Ameacha mjane, Saada Ibrahim na watoto wanne,  Laila aliyezaliwa 1994, Zahra mwaka 1996, Sophia mwaka 1997 na wa mwisho Abdulrazak aliyezaliwa mwaka 2002.