VIDEO: Alichokisema Gwajima kuhusu video inayosambaa mtandaoni

Muktasari:

Kama umesikia kuhusu kusambaa kwa video ya ngono inayomuonyesha mtu mwenye sura inayofanana na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akiwa faragha na mwanamke ambaye bado hajajulikana, basi leo Jumatano Mei 8, 2019 kiongozi huyo wa kiroho amesema si yake, na imewekwa na watu wanaolenga kumchafua.

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima ametoa ufafanuzi kuhusu video ya ngono inayosambaa mtandaoni ikimuonyesha mtu mwenye sura kama yake akiwa faragha na mwanamke ambaye bado hajafahamika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Mei 8, 2019, Askofu Gwajima amesema video hiyo si yake, akibainisha kuwa imetengenezwa kwa lengo la kumchafua na kumnyamazisha.

Amebainisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2020 umekaribia hivyo kuna watu wamedhamiria kumnyamazisha ila ukweli ni kwamba video hiyo haitamrudisha nyuma.

“Najua kuna watu wanajaribu kunichafua na kuninyamazisha kuelekea uchaguzi mkuu sasa nawammbia mdomo huu haunyamazishwi.”

“Nimefuatilia namjua aliye nyuma na video ile na nimeanza kufuatilia, tayari nimeripoti polisi na nimetoa taarifa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) wamtafute na ninataka nione kama kweli sheria ya mtandao inafanya kazi,” amesema Gwajima.

Gwajima amemuonya aliyetengeneza video hiyo na kumtaka kufanya anayotakiwa kufanya kinyume na hapo ataanza kumshughulikia kanisani kwake kuanzia Jumapili Mei 12, 2019.