VIDEO: Alichokisema Lugola baada ya kuambiwa na Magufuli kuwa hafai

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema ataendelea kumsaidia Rais John Magufuli   kwa kuwa yeye ni mbunge wa Mwibara (CCM).

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema ataendelea kumsaidia Rais John Magufuli   kwa kuwa yeye ni mbunge wa Mwibara (CCM).

Lugola ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 23, 2020  jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumalizika hafla ya uzinduzi wa nyumba za  maofisa wa Jeshi la Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.

Alieleza hayo baada ya Rais John Magufuli  ambaye wakati akizungumza  katika uzinduzi huo kusema Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias  Andengenye hawafai kuendelea na nyadhifa zao kutokana na mambo waliyoyafanya kuhusu uingiaji wa mikataba.

“Nitaendelea kuwapenda lakini kwenye nafasi zenu hapana. Watanzania mmenichagua kusimamia haki na utendaji kazi ndani ya Serikali ili kila fedha ya Watanzania iktumike kwa mujibu wa sheria,” amesema Rais Magufuli.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Rais na nini maoni yake,  Lugola amesema yeye ni mbunge ataendelea kumsaidia Rais na Serikali.

"Rais ndiyo aliniteua kwenye baraza lake la mawaziri na Rais ndiyo ameona anipumzishe kwenye baraza la mawaziri. Kwangu mimi ni jambo la faraja na hatua aliyoichukua...,ni hatua nzuri inayolenga kujenga vizuri safu ya Serikali.”

"Mimi ni mbunge nitaendelea kumsaidia Rais kwa heshima kubwa," amesema Lugola.

Kabla ya Rais Magufuli kueleza kuhusu mikataba hiyo, alifika katika hafla hiyo akiwa ameambatana na Lugola na viongozi wengine na kukaa naye meza kuu.

Baada ya hafla hiyo kuisha, Lugola alikuwa wa mwisho kushuka jukwaa kuu akiwa ameongozana na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba.

Aliondoka eneo hilo na gari la Serikali analolitumia tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

 

Alichokisema Magufuli

Magufuli amesema kutokana na sakata hilo katibu mkuu wa wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu ameandika  barua ya kujiuzulu na amemkubalia.

“Watu wamekosa uadilifu, hivi karibuni kulikuwa na mkataba mmoja wa ajabu unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya  zaidi ya Sh1 trilioni. Mradi huo umesainiwa na kamishna jenerali wa Zimamoto.”

“Haujapangwa kwenye bajeti na haujapitishwa na Bunge. Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wote wa Tanzania waliokuwa wanakwenda katika majadiliano na kulipwa Dola 800 za posho ya vikao,” amesema Magufuli, na kubainisha kuwa hata tiketi za ndege walilipiwa.

Amesema mkataba huo ni wa hovyo kwa sababu ili kuuvunja yaliyoanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa.

“Lugola nampenda sana ni mwanafunzi wangu nimemfundisha Sengerema Sekondari pamoja na mwili na ukubwa wake lakini katika hili hapana. Nilitegemea hata hapa sitamkuta, nasema kwa dhati.”

“Andengenye nampenda sana, ni mchapakazi lakini kwenye hili hapana, nilitegemea asiwepo hapa. Hatuwezi kuendesha nchi kwa misingi ya ajabu namna hii. Yanayokwenda kununuliwa katika mkataba ni ya hovyo.”

Ameongeza, “nampongeza Kingu kwa kuwajibika na hii imempa heshima kwamba angalau ametambua, inawezekana haya hakuyafanya yeye lakini kwa kuwa yeye ni katibu mkuu amewajibika kwa hilo, nampongeza na nitaendelea kumheshimu.”

Magufuli ameshangazwa mtu kusaini Sh1 trilioni wakati jukumu la kukopa fedha ni la Wizara ya Fedha.

Amesema haiwezekani watendaji kufanya mambo wanavyotaka kwa kuwa wataipeleka nchi kubaya na kukiuka misingi na ilani ya uchaguzi ya CCM.

“Huo ndio ukweli na siku zote nitasimamia ukweli, Ndugu zangu ninajua hili…, wapo pia ofisi ya mwanasheria mkuu, walisubiri mwanasheria mkuu alipofiwa na mke wake wakaenda wakapitisha na kuandika kwa niaba na kwa niaba, wapo nao wanahusika.”

“Wapo wanaohusika katika wizara ya Mambo ya Ndani lakini kitendo cha Zimamoto na ni wasaidizi wa Andengenye ni lazima wajitathmini,” amesema Magufuli