Alichokisema Lugola kuhusu wahamiaji haramu

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amewataka wanaoishi nchini kinyume na taratibu kufika katika ofisi za Idara ya Uhamiaji zilizopo katika maeneo wanayoishi kabla hawajabainika.

Moshi. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amewataka wanaoishi nchini kinyume na taratibu kufika katika ofisi za Idara ya Uhamiaji zilizopo katika maeneo wanayoishi kabla hawajabainika.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 31, 2019 mjini Moshi mkoani Kilimanjaro  wakati akifungua kikao cha maofisa uhamiaji waandamizi wa Tanzania Bara na Zanzibar, kusisitiza kuwa Serikali ipo makini.

“Kupitia mkutano huu nitume salamu kwa mhamiaji haramu anayejijua hajafuata utaratibu wa kuwa nchini. Ajisalimishe mwenyewe katika ofisi ya uhamiaji iliyopo karibu naye,” amesema.

Lugola amempongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala kwa kuanzisha mkakati mzuri wa kuwasaka wahamiaji hao, kwamba wizara yake itashirikiana na idara hiyo kuhakikisha zoezi hilo linafanyika vizuri.

Kwa upande wake Makakala amesema idara hiyo imepata mafanikio mbalimbali na kwa sasa wapo mbioni kuzindua udhibiti mpakani mipaka kwa njia ya kielektroniki, hatua itakayosaidia kudhibiti mipaka na kuongeza mapato.