Alichokisema Lugola saa chache kabla ya kutumbuliwa

Muktasari:

Jana mchana Alhamisi Januari 23, 2020 katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi alitangaza mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais John Magufuli.

Dar es Salaam. Jana mchana Alhamisi Januari 23, 2020 katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi alitangaza mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais John Magufuli.

Mabadiliko hayo yalifanyika saa chache baada ya Magufuli kueleza kasoro iliyofanyika katika mkataba akimhusisha aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye na Lugola aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Magufuli alieleza hayo katika hafla ya uzinduzi wa nyumba za maofisa wa Jeshi la Magereza, Ukonga Dar es Salaam, kueleza kuwa Lugola na Andengeye wamefanya mambo mazuri lakini kutokana na kasoro hizo za mikataba, hawafai kuendelea na nyadhifa zao.

Baadaye mchana Balozi Kijazi alisoma mabadiliko yaliyofanywa na Magufuli aliyemteua George Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mussa Azzan Zungu kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Katika hafla ya uzinduzi wa nyumba hizo, Lugola aliwataka Watanzania kusifu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

“Siku za Serikali ya Awamu Tano zinahesabika, nikwambie mheshimiwa Rais  Watanzania wanaokuunga mkono ni asilimia 99.1, hao waliobaki ni wale mioyo yao imeshikiliwa na adui shetani na ni wachache nawakemea washindwe.”

“Kwa kuwa katika kipindi hiki Watanzania wamekuweka juu ukang’ara, itakula kwao utaendelea kuwa juu na juu zaidi. Siku mkibeza juhudi hizi zinazofanywa, amani  ikakatika fedha zote mheshimiwa rais atazielekeza kununua risasi, mabomu kwa ajili ya kulinda nchi matokeo yake hatutajenga hospitali wala watu kulima na mwisho nchi itakuwa masikini.”