Alichokisema Padri Sabuni ibada mazishi ya Mwanakotide

Wanachama wa chadema wakiutoa mwili wa marehemu, Fulgency Mapunda maarufu ‘Mwanakotide’ katika kanisa katoliki parokia ya moyo mtakatifu wa yesu lililopo Manzese jijini Dar es Salaam leo, baada ya misa ya kumuaga iliyofanyika kanisani hapo. Mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda mkoani Ruvuma kwa ajili ya maziko. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Padri Paul Sabuni wa Kanisa Katoliki Manzese amewataka watu  kutenda mema ili siku wakifariki dunia washangiliwe kwa kuwa watakwenda mahali salama.

Dar es Salaam. Padri Paul Sabuni wa Kanisa Katoliki Manzese amewataka watu  kutenda mema ili siku wakifariki dunia washangiliwe kwa kuwa watakwenda mahali salama.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 9, 2019 katika ibada  ya mazishi ya kada wa Chadema, Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide aliyefariki Dunia Jumapili Oktoba 6, 2019 katika Hospitali ya Mtakatifu Monica, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.

Amesema anashangazwa kuona watu wakilia mtu akifariki kwa maelezo kuwa wanadhani amekwenda sehemu mbaya, badala yake amewataka kufurahia maisha ya Mapunda kwa sababu amepata fursa ya kuagwa katika kanisa hilo ikiwa ni ishara kuwa alitenda mema.

"Mtu anapokufa katika mikono ya Mungu tunapaswa kumshangilia Mungu, tunapaswa kumshangilia marehemu wetu, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa zawadi aliyotupa kwa maisha ya mpendwa wetu," amesema Padri Sabuni.

Amesema kulia katika msiba huo ni kukosa shukrani kwa Mungu kwa miaka 42 ya Mapunda.

Amebainisha kuwa wazazi wanaojifungua watoto wanaofariki dunia ndio wanastahili kulia zaidi.

"Ndugu waumini tutendeni matendo mema, hakuna hata mmoja wetu, sio mimi padri wenu sio Baba Mtakatifu, sisi wote ni wenye dhambi  tunahitaji huruma ya Mungu," amesema padri huyo.

Amewapongeza Chadema kwa kuendelea kumthamini Mapunda hata baada ya kuwa amefariki, kuwataka kuendelea  kuiangalia familia yake kwa sababu walikuwa wakimtegemea katika masuala mbalimbali.