Aliyefungwa miaka 20 kwa kulawiti, ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kesi nyingine ya mauaji

Sunday September 15 2019

 

By Daniel Mjema,Mwananchi [email protected]

Moshi. Mkazi wa Kaloleni mjini Moshi, Mariki Ulomi (50) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 11 na kusababisha kifo chake.

Tayari Ulomi anatumikia kifungo kingine cha miaka 20 jela kwa kosa la kulawiti alilokutwa na hatia katika kesi ya jinai namba 70/2015.

Anatuhumiwa kutenda kosa la mauaji wakati akiwa nje kwa dhamana katika kesi namba 70/2015.

Mshitakiwa huyo, ambaye jana alifika mahakamani akitokea gerezani ambako anatumikia kifungo hicho, alijikuta akihukumiwa kunyongwa hadi kufa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Fauz Twaibu kutokana na kosa la mauaji.

Awali mawakili wa Serikali kutoka Divisheni ya Taifa ya Mashitaka (NPS)-- Kassim Nassir na Nitike Emanuel-- walidai kuwa Mei 23, 2015, mshitakiwa alimuua kwa makusudi Fraterin Massawe, mtoto mwenye umri wa miaka 11.

Mwili wa mtoto huyo, aliyekuwa akiishi na wazazi wake eneo la Karanga Katanini, ulikutwa katika shamba la Masista Katanini, ukiwa umevuliwa bukta na pia ukionekana kutokwa na haja kubwa.

Advertisement

Akisoma hukumu jana, Jaji Twaibu alisema mashahidi sita wa upande wa mashitaka, wamethibitisha shitaka hilo kwa kuegemea ushahidi wa mazingira.

Jaji Twaibu alisema ushahidi unaonyesha mshitakiwa alikuwa wa mwisho kuonekana na mtoto huyo na pia hakueleza ni namna gani aliachana naye zaidi ya kukanusha kuhusika na mauaji.

Baada ya kumtia hatiani, mawakili wa NPS walioendesha kesi hiyo walimuomba Jaji ampe mshitakiwa adhabu kwa mujibu wa sheria na ndipo alipomhukumu mshitakiwa adhabu ya kifo.

Hivi ndivyo ushahidi ulivyokuwa

Mei 21,2015, saa 9:00 mchana, kaka wa marehemu aitwaye, Justine Massawe akiwa chumbani kwake, alimsikia mdogo wake na alipochungulia dirishani aliona anaongea na mshitakiwa.

Baada ya kuona mdogo wake alikuwa akiongea na mtu anayemfahamu, hakuwa na wasiwasi na akaendelea kulala hadi ilipofika saa 11:30 jioni alipoamka na kukuta mlango wake umefungwa kwa nje.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, kaka wa marehemu alivunja mlango huo na kutoka nje lakini hakumuona mdogo wake na baadaye alimjulisha baba yake, Theodore Massawe.

Baba huyo alimtafuta mwanae hadi usiku bila mafanikio na kuamua kutoa taarifa polisi Mei 22,2015 kuhusu kupotelewa na mtoto lakini wakati huo wakiendelea kumtafuta.

Siku iliyofuata, mzazi akapata wazo kuwa pengine amtafute mwanae kijiji cha jirani na wakati akielekea huko akiwa na mbwa wake, walipofika shamba la Masisita mbwa wake akawa anamzuia.

Akaona mbwa wake anaelekea katika shamba hilo na alipomfuata, mbele kidogo akaona viatu vyake (mzazi) na wakati anajiuliza vimefikaje huko ndipo alipouona mwili wa mwanae.

Mwili wa mwanae, ambaye alikuwa akisoma darasa la nne shule ya msingi Magereza, ulikutwa ukiwa umelalia tumbo huku ukiwa umevuliwa bukta na pia ukiwa umetokwa na haja kubwa.

Baba mzazi alimshuku mshitakiwa kutokana na kukabiliwa na tuhuma za ulawiti na ubakaji na polisi walipomtafuta nyumbani kwake Kibosho Road, hakupatikana hadi alipokamatwa Kaloleni.

Baada ya mtuhumiwa kufanya tukio hilo alihama eneo alilokuwa akiishi Kibosho Road na kuhamia Kaloleni katika Manispaa ya Moshi, hadi alipokamatwa.

Advertisement