VIDEO: Aliyekuwa mkurugenzi Takukuru alala mahabusu, kufikishwa mahakamani leo

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo

Muktasari:

Yule kigogo wa Takukuru aliyekuwa mkurugenzi wa mipango, ufuatiliaji na tathmini Kulthum Mansoor anayedaiwa kuwadhulumu viwanja wafanyakazi wa taasisi hiyo amekamatwa na polisi, leo atafikishwa mahakamani

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor anayetuhumiwa kuwadhulumu viwanja wafanyakazi wa taasisi hiyo, amekamatwa na polisi.

Kulthum amekamatwa jana Alhamisi Machi 28, 2019 na kupelekwa kituo cha polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 29, 2019, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema, “Ni kweli amekamatwa jana na yuko Oysterbay na leo atafikishwa mahakamani.”

Mbungo amesema wakati jana Rais John Magufuli anamzungumzia kigogo huyo, uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili ulikuwa umefikia mwisho.

“Jana wakati Rais anazungumzia, uchunguzi ulikuwa umeanza  na alikamatwa  na kulala mahabusu na leo kama nilivyosema atafikishwa mahakamani,” amesema Mbungo.

Jana,  Rais Magufuli  akizungumza Ikulu mara baada ya kumuapisha Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola pamoja na kupokea ripoti ya Takukuru alisema anashangazwa kwa taasisi hiyo kutomchukulia hatua.

“Kuna mkurugenzi mmoja pale makao makuu amewauzia viwanja hewa wafanyakazi wenzake vya zaidi ya Sh1 bilioni lakini hajapelekwa mahakamani,” amesema Magufuli.

“Wala sijapata taarifa hizo hela amezirudisha kwa wafanyakazi aliowadhulumu, wale wafanyakazi wameshindwa kumdai kwa sababu ni bosi wao, wanaumia, wanalalamika pembeni. Amewadanganya kwamba ana viwanja kule Bagamoyo, mpaka leo hawajapewa.”

 

Ameongeza, “Sasa najiuliza haya Takukuru ni wa watu wengine?  Hoja iko wazi  anarudisha hela haraka au anafikishwa mahakamani.”