Aliyekuwa mkurugenzi Takukuru apandishwa mahakamani

Aliekuwa Mkurugenzi wa mipango,ufwatiliaji na tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru) Kulthumu Mansoor akiwa katika Mahaka ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Muktasari:

Leo Ijumaa aliyekuwa mkurugenzi wa mipango, ufuatiliaji na tathmini Kulthum Mansoor anayedaiwa kuwadhulumu viwanja wafanyakazi wa taasisi hiyo amepandishwa Mahakama ya Kisutu kujibu tuhuma zinazomkabili

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na makosa manane likiwemo la utakatishaji wa fedha wa Sh1,477, 243,000

Kulthum amepandishwa kizimbani leo Ijumaa Machi 29, 2019 akitokea kituo cha polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam ambako alikuwa mahabusu toka jana Alhamisi alipokamatwa kwa tuhuma hizo.

Kigogo huyo amepandishwa mahakamani ikiwa ni siku moja imepita tangu Rais John Magufuli alipoutaka uongozi wa Takukuru kueleza wamefikia wapi kuhusu mtumishi wao ambaye amekuwa akilalamikiwa na wafanyakazi kwa kuwauzia viwanja hewa watumishi wenzake.

Rais Magufuli akizungumza Ikulu jana mara baada ya kumuapisha Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola pamoja na kupokea ripoti ya Takukuru alisema anashangazwa kwa taasisi hiyo kutomchukulia hatua.

“Kuna mkurugenzi mmoja pale makao makuu amewauzia viwanja hewa wafanyakazi wenzake vya zaidi ya Sh1 bilioni lakini hajapelekwa mahakamani,” amesema Magufuli.

“Wala sijapata taarifa hizo hela amezirudisha kwa wafanyakazi aliowadhulumu, wale wafanyakazi wameshindwa kumdai kwa sababu ni bosi wao, wanaumia, wanalalamika pembeni. Amewadanganya kwamba ana viwanja kule Bagamoyo, mpaka leo hawajapewa.”

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea mahakamani hapo