Aliyekuwa mkurugenzi Takukuru asomewa mashtaka manane

Muktasari:

Aliyekuwa mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji na Tathmini wa Takukuru amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka nane likiwemo la utakatishaji fedha Sh1.4bilioni.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka manane likiwemo la utakatishaji wa Sh1.4bilioni.

Wakli wa Serikali, Simon Wankyo akisoma hati ya mashtaka leo Ijumaa Machi 29, 2019 mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina amedai Kulthum anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.

Wankyo amedai katika kosa la kwanza la kughushi tarehe tofauti Januari 2013 na Mei 2018 akiwa Makao Makuu ya Takukuru jijini Dar es Salaam, alitoa barua ya ofa ikionyesha barua hiyo imetoka halmashauri ya Bagamoyo huku akifahamu kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Kosa la pili hadi la saba, tarehe tofauti kati ya Januari 2012 na Mei 2017 akiwa eneo la Upanga mshtakiwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh 1.477,243,000 kutoka kwa watumishi sita wa Takukuru, kama malipo ya viwanja vilivyopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wakati akijua ni uongo.

Katika kosa la nane la utakatishaji fedha, tarehe tofauti kati ya Januari 2013 na Mei 2018 akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia Sh1.477,243,000 huku akijua fedha hizo ni zao la makosa mengine.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo. Wankyo amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe ya kutajwa.

Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 12, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.