Aliyekwepa karantini akamatwa Dodoma

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi

Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amesema amemkamata raia mmoja wa Marekani mwenye asili ya Tanzania anayedaiwa kuingia nchini wiki nne zilizopita akimtuhumu kukwepa karantini ya siku 14.

Serikali iliagiza watu wote watakaoingia nchini kuanzia Machi 20 wakae katika karantini ya siku 14 ili kujiridhisha kama hawana maambukizi ya virusi vya corona.

Raia huyo alikamatwa juzi akiwa katika bodaboda jijini hapa baada ya kuingilia msafara wa viongozi.

Katambi alisema Serikali lazima ifanye uchunguzi dhidi ya raia huyo na hivyo amemuweka chini ya uangalizi wa timu ya wataalamu wa afya kwa ajili ya uchunguzi.

“Alijitetea kuwa alijiweka karantini siku 14 nyumbani kwao, lakini hatuwezi kuyaamini maneno yake, hivyo lazima wataalamu wa afya wamchunguze,” alisema Katambi.

Akijitetea mbele ya Katambi baada ya kukamatwa, mtu huyo alijitetea. “Nyumbani kuna chumba maalumu kwa ajili ya mtu kujihifadhi, hivyo nilivyoingia nchini nilijiweka karantini siku 14, baada ya hapo ndipo nikatoka nje,” alisema lakini Katambi hakumwamini na kuagiza awekwe chini ya uangalizi.

Katambi pia alimtaka mchekeshaji maarufu Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ afike ofisini kwake akimtuhumu kufanyia mzaha ugonjwa huo, baada ya watu aliowahoji kuonyesha kuwa hawajui Covid-19 ni nini. Hata hivyo hakuna hatua zilizotangazwa baada ya wawili hao kukutana.

Hilo ni tukio la pili, Aprili 3, 2020, polisi wa Iringa walimkamata mtu mmoja ikidaiwa alitoroka karantini Dar es Salaam siku tatu tangu awasili nchini akitokea Norway.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema alipata taarifa kwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Daniel Chongolo na kuamua kumfuatilia.

“Tuliwasiliana na polisi, na kujua nyumba anayokaa na nikaongea na mganga mkuu, ametoa wataalamu tumemchukua na kumuweka karantini,” alisema na kuhimiza umakini maeneo yenye karantini.

Wakati huo huo, Serikali imetangaza rasmi kuwa wasafiri wote wanaoingia nchini kutoka nchi zilizoathirika na corona watalazimika kukaa karantini kwa siku 14 katika hosteli za wanafunzi za Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam zinazoitwa Dk John Magufuli.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema jana wasafiri hao watafikia katika hosteli hizo zilizopo eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwepo udhibiti wa kutosha wa mienendo ya wasafiri hao.

“Tumeona taarifa za Iringa, kuna baadhi ya wasafiri tuliwaweka hotelini wakatoroka sasa ili kudhibiti mienendo ya wasafiri hawa na kuwalinda Watanzania wengi tumeona upo ulazima wa kuwaweka sehemu moja kwenye ulinzi wa saa 24,’’ alisema.