Aliyemuua mwanaye aachiwa huru Tanzania

Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imemwachia huru Mtonya Magana (74) baada ya kukutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia mwanaye, Julius Mchiwa wakati akiamua ugomvi kati ya mtoto huyo na mama yake mzazi.

Hakimu Mkuu Mfawidhi, Dainess Lyimo alisema Mahakama hiyo imeamua kumwachia huru mshtakiwa kutokana na mazingira ya tukio yalivyokuwa.

Lyimo alisema kutokana na hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani marehemu Mchiwa alianzisha ugomvi na familia yake uliosababisha kifo chake mwenyewe.

“Hivyo ninakuachia huru kuanzia sasa lakini usitende kosa lolote la jinai ndani ya kipindi cha miezi 12 kuanzia sasa,” alisema Hakimu Lyimo.

Awali, Mwanasheria wa Serikali, Bertha Kulwa aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 18, 2016.

Kulwa alisema Mchiwa alikuwa na ugomvi na mkewe anayeitwa Salome Mwaluko na chanzo cha ugomvi huo ni Mchiwa kutaka kuwachukua watoto wake kutoka kwa mkewe huyo ambaye walishaachana.

(Rachel Chibwete)