Aliyemwandikia barua DPP kukiri shtaka, ahukumiwa

Friday September 27 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania, imemhukumu raia wa Sri Lanka, Abdul  Amaan (26) kulipa faini ya Sh10 milioni au kwenda jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha madini aina tisa yakiwemo ya Tanzanite, bila kuwa na kibali.

Amaan ambaye ni mwanafunzi, amehukumiwa kifungo hicho leo Ijumaa  Septemba 27, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kukiri shtaka la kusafirisha madini hayo yenye thamani ya zaidi ya Sh30 milioni.

Pia, mahakama hiyo imetaifisha madini yote aliyokuwa akifirisha mshitakiwa huyo bila kuwa na kibali.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Simba amesema mshtakiwa ametiwa hatiani baada ya kukiri shtaka lake.

"Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa, hivyo unatakiwa kulipa faini ya Sh10 milioni na kama mshtakiwa utashindwa kulipa faini hii, basi utatumikia kifungo cha miaka mitatu jela" amesema Hakimu Simba

" Pia, madini aliyokutwa nayo mshtakiwa huyu, mahakama hii imeyataifisha na kuwa mali ya Serikali," amesema Simba.

Advertisement

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Jackline Nyantori ameiomba mahakama hiyo, itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa hiyo.

"Naiomba mahakama hii itoe adhabu kali dhidi ya Amaan  kwa sababu usafirishaji wa madini bila kuwa na kibali unapunguza pato la taifa ambalo lingeweza kutumika katika shughuli nyingine za kijamii," amedai Wakili Nyantori.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa mshtakiwa huyo kujitetea, ambapo aliomba mahakama isimpe adhabu kali kwakuwa anategemewa na familia yake.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo , Septemba 26, 2019 akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Amaan baada ya kusomewa shtaka lake, wakili wake Shabani Mlembe aliieleza mahakama hiyo kuwa  tayari wameshamuandikia  barua Mkurugenzi wa Mashtaka wa Tanzania (DPP) kukiri kosa hilo na kwamba wanaomba mahakama ipange  tarehe ya karibu ili kufanya utaratibu unaotakiwa kisheria.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Septemba 21, 2019  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Siku hiyo ya tukio, Amaan alikutwa akisafirisha madini aina ya Scapolite yenye uzito wa gramu 996.50;  Sperssartite gramu 487;  Tanzanite gramu 44; Quarts gramu 126; Citrine gramu 174; blue agate gramu 101.80; Toumarine gramu 16;  Aquamarine gramu 14.30 na Supphire gramu 5.04 yote yakiwa na thamani ya Sh 36.5 milioni, bila kuwa na kibali wala leseni kutoka mamlaka husika.

Advertisement