Aliyeshika nafasi ya pili kitaifa darasa la saba, hakusoma darasa la kwanza

Francis Gwagi ambae ni mwanafunzi bora wa kiume na wa pili kitaifa kutoka shule ya msingi Paradise akiwa amebebwa na baba yake Hussein Gwagi nyumbani kwao Katoro wilayani Geita

Muktasari:

  • Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza matokeo ya mtihani ya darasa la saba ya mwaka 2019 ambapo mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kwa wavulana kitaifa na nafasi ya pili kitaifa hakusoma darasa la kwanza.

Geita. Wakati wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka 2019 wakiwa wamesoma miaka saba, hali ni tofauti kwa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa upande wa wavulana na nafasi ya pili kitaifa.

Mwanafunzi huyo Francis Gwagi (14)amesoma miaka sita baada ya kuvushwa darasa la kwanza kutokana na kuonekana kuwa na akili zaidi.

Francis aliyekua mwanafunzi wa shule ya msingi Paradise amesema hayo leo Jumanne Oktoba 15, 2019 alipokuwa akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao Katoro mkoani Geita muda mfupi baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Amesema toka ameanza shule haijawahi kukosa namba moja kwenye mitihani yake.

Baba mzazi wa Francis, Hussein Gwagi amesema ni neema ya Mungu kwa kumpa watoto wenye akili kwakua kwenye familia yao hakujawahi kuwa hata na mwalimu

"Mimi ni mkulima kwetu hatujasoma zaidi ya darasa la saba, kwenye ukoo wetu hatujawahi kuwa hata na mwalimu na mshukuru Mungu ameisaidia familia yangu mke wangu ni muombaji sana,” amesema

“Dada yake huyu yupo Msalato na tuliambiwa huyu kwakua ni wa kwanza wa kiume ajitahidi maana ndie kiongozi wa familia na kweli Mungu ametusikia," amesema Hussein