Aliyetoka gerezani kwa ugaidi achoma watu visu jijini London

Muktasari:

Aua watu wawili na kujeruhiwa wengine watatu


London, Uingereza. Mtu mmoja aliyetoka gerezani kwa makosa ya ugaidi amewachoma visu watu watano jijini London, Uingereza.

Mshambuliaji Usman Khan (28) aliachiwa kutoka gerezani mwaka jana alikokuwa anatumikia kifungo kwa makosa ya ugaidi tangu 2012.

Khan alifanya shambulio hilo jana saa 8:00 mchana katikati ya jiji, karibu na daraja la London, tukio linaloelezwa kuwa la kigaidi.

Polisi mjini London wamesema watu wawili waliochomwa kisu na Khan wamefariki dunia na wengine watatu wanatibiwa hospitalini.

Hata hivyo, baada ya kutekeleza unyama huo unaoelezwa na mamlaka za London kuwa ni ugaidi,  polisi walimuua mtuhumiwa huyo kwa risasi.

“Mtuhumiwa wa kiume ameuawa na wataalamu wa udunguaji kutoka Polisi wa Jiji la London, na ninaweza kuthibitisha kuwa alikufa palepale katika eneo la tukio,” alisema Neil Basu, ofisa anayeshughulika na masuala ya ugaidi.

Kufuatia tukio hilo, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema  ni muhimu kwa nchi hiyo kutekeleza adhabu mahususi za ugaidi.

“Ni kosa kuruhusu wahalifu wakubwa na wasiotulia kutoka magerezani mapema, ni lazima kuachana na mchezo huo na kuanza kutekeleza adhabu zinazostahiki kwa wahalifu hatari, hasa magaidi,” alisema Johnson.

Mkuu wa Polisi ya London, Cressida Dick amesema waathirika wawili waliochomwa kisu walifariki dunia na wengine watatu waliojeruhiwa wanatibiwa hospitalini.