Anayedaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh15 milioni adakwa akiwa msibani

Muktasari:

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) mjini Dodoma imemkamata mratibu  wa mradi wa Belgian Fund for Food Security (BFFS) Wilaya ya Bahi, Emmanuel Mziwanda (62) kwa tuhuma za kuisababisha Serikali hasara ya Sh15 milioni.

Dodoma. Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) mjini Dodoma imemkamata mratibu  wa mradi wa Belgian Fund for Food Security (BFFS) Wilaya ya Bahi, Emmanuel Mziwanda (62) kwa tuhuma za kuisababisha Serikali hasara ya Sh15 milioni.

Mkuu wa taasisi hiyo mjini humo, Sosthenes Kibwengo akizungumza leo Jumanne Oktoba Mosi, 2019 amesema mtuhumiwa huyo aliyekamatwa akiwa msibani alikuwa akitafutwa na taasisi hiyo tangu Julai,  2017 akikabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka na kumdanganya mwajiri wake.

Amesema kitendo hicho kimeisababishia Serikali hasara ya Sh15 milioni na kwamba baada ya uchunguzi kukamilika  na mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kutoa kibali cha kumfikisha mahakamani, mtuhumiwa alitoweka kusikojulikana.

“Mziwanda alitoweka hadi tulipomkamata Septemba mwaka huu akiwa msibani Wilaya na Mpwapwa Mkoani Dodoma, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma dhidi yake baada ya taratibu za kisheria kukamilika. Tunashukuru wote waliotoa ushirikiano,” amesema Kibwengo.